Jumapili, 25 Novemba, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfungo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria, sawa na tarehe 25 Novemba, 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1493 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko masaa mengi akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Malaika Jibril alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.
Siku kama hii ya leo miaka 1357 iliyopita, sawa na terehe 17 Rabiul Awwal mwaka 83 Hijiria alizaliwa pia mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii miwili adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa tishio kwa maslahi ya taifa.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi hiyo kupitia mapinduzi ya uwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo aliyoitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jeusi la ukatili na mauaji.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita yaani sawa na tarehe 25 Novemba 1975, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic.
Siku kama ya leo miaka saba iliyopita alifariki dunia Vasiliy Ivanovich Alekseyev, bingwa mnyanyuaji uzani wa nchini Russia na kimataifa. Alekseyev alipata ushindi mwaka 1972 mjini Munich, Ujerumani na mwaka 1976 Montréa, Canada kwa kujinyakulia medali za dhahabu. Katika kipindi cha ushindi wake, Vasiliy Ivanovich Alekseyev aliweka rekodi ya dunia. Yeye alikuwa mnyanyuaji uzani ambaye aliweza kuweka rekodi ya kunyanyua kilogramu 645 kwa kupindukia kilogramu 600. Mwaka 1993 Shirikisho la wanyanyuaji uzani duniani lilimteua Alekseyev kuwa mmoja wa mabingwa wakubwa katika fani hiyo. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 nchini Ujerumani kutokana na matatizo ya moyo.