Jumatano tarehe 28 Novemba, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 28 mwaka 2018.
Siku kama ya leo miaka 990 iliyopita yaani tareher 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 450 Hijria, alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari, aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi Sima'a" na "al Ghinaa wa Al Ta'aliqatil Kubra fil Furu'u.

Siku kama ya leo miaka 261 iliyopita, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza. Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb.

Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 yaani miaka 198 iliyopita, alizaliwa Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, nchi ya Albania ilipata uhuru. Nchi hiyo ilikuwa huru miaka mingi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, lakini baada ya kuasisiwa ufalme wa Roma ilikaliwa kwa mabavu na utawala huo. Mwaka 1501 Albania ilidhibitiwa na utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 19 utawala huo ulidhoofika na kupoteza nchi za Balkan ilizokuwa ikizitawala na kwa juhudi za wapigania uhuru, hatimaye mwaka 1912 Albania ikajipatia uhuru.

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15. Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini Miladia, wananchi wa Mauritania walishiriki kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa Jamhuri yenye mamlaka ya ndani. Hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa.

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo Iran ilidhibiti visiwa vitatu vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Bu Musa baada ya kuondoka vikosi vamizi vya Uingereza katika maeneo hayo. Uingereza iliondoka katika visiwa hivyo vitatu vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi katika fremu ya mpango wa nchi hiyo wa kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Bahari ya Mediterranean na Ghuba ya Uajemi kutokana na matatizo ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua nchi hiyo.

Na katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, vikosi vya Jeshi la Majini la Iran vilifanya operesheni katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kufanikiwa kuvisambaratisha vikosi vya majini vya jeshi la Iraq. Tukio hilo lilitokea takribani miezi miwili tu baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran. Operesheni hiyo ilipelekea kutokea mapigano makali kati ya meli za kivita za pande mbili na meli nyingi za kivita za Iraq ziliteketezwa. Kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa vikosi vya majini katika operesheni hiyo, siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la “Siku ya Jeshi la Majini”.
