Dec 03, 2018 01:05 UTC
  • Jumatatu, 3 Disemba, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 25 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Disemba 3 mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1004 iliyopia sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Ali Bin Hussein Baghdadi maarufu kama Sayyid Murtadha fakihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Sayyid Murtadha aliyejulikana pia kwa lakabu ya A'lamul Huda. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za fasihi ya Kiarabu, mantiki na mashairi na kwa miaka 30 alihukumu mjini Baghdad. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20.

Sayyid Murtadha A'lamul Huda

Katika siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafalsafa wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajenda Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru wa nchi hiyo na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. 

Dakta Rajendra Prasad

Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, Auguste Renoir mchoraji mkubwa wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Renoir alizaliwa tarehe 7 Machi 1841 na kwa haraka mno aliweza kuonyesha dhuku na mapenzi yake kwa taaluma ya uchoraji. Akiwa na umri wa miaka 19 tayari Auguste Renoir alikuwa ameshaondokea kuwa mchoraji mahiri na mashuhuri mjini Paris.

Auguste Renoir

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsiya, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. 

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama ulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Maelfu ya wakazi mji wa Bhopal walipoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa katika janga hilo ambalo lilitambuliwa kuwa janga kubwa zaidi la viwandani duniani. 

janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda Bhopal

Na miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kombora la balestiki