Dec 11, 2018 02:34 UTC
  • Jumanne, Disemba 11, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 3 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 11, 2018.

Tarehe 11 Disemba miaka 175 iliyopita alizaliwa daktari na mtaalamu wa vijidudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu,  Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutiwa wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.

Robert Koch

Miaka 148 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1292 Hijiria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Qasim Kalantari. Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa Tehran. Ayatullah Kalantari alibobea sana katika elimu za hadithi, falsafa na mantiki. Msomi huyo alipata elimu kwa wasomi mashuhuri wa mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq akiwemo Shekh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya Ijtihad. Ameandika vitabu vingi hasa katika uwanja wa fiqhi na sheria za Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, aliuawa shahidi Ayatullah Sayyid Abdulhussein Dastgheib, alimu mkubwa na mwalimu wa akhlaq wa Kiislamu. Ayatullah Dastgheib aliuawa shahidi na kundi la munafiqin alipokuwa akielekea kwenye Swala ya Ijumaa. Alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran na alipata elimu yake ya kidini hadi daraja ya ijtihadi katika chuo cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Dastgheib pia alishirikiana na maulamaa wengine waliokuwa na mwamko na wanaharakati wa Iran katika kufundisha elimu ya Kiislamu, kupambana na utawala wa Shah na mara kadhaa alikamatwa na kufungwa jela. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Madhambi Makubwa", "Maad" pamoja na tafsiri ya sura kadhaa za Qur'ani Tukufu.'

Ayatullah Sayyid Abdulhussein Dastgheib

Na tarehe 11 Disemba inatambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa na kutangazwa Jamhuri ya Burkina Faso. Nchi hiyo ilikoloniwa na Ufaransa kuanzia katikati mwa karne 19. Burkina Faso ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Upper Volta, ilijitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake ya ndani mwaka 1958 baada ya kutangazwa mfumo wa jamhuri lakini ilibakia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ufaransa. 

Bendera ya Burkina Faso