Dec 17, 2018 18:52 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (134)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji tunapokutana tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

 

 Kipindi chetu kilichopita kiliendelea kuzungumzia maudhui ya toba na kutubia dhambi. Tulibainisha kwamba, uwepo wa toba na mlango wa kutubia dhambi sambamba na mja kuwa na azma na irada thabiti ya kuacha dhambi na kufanya harakati kuelekea upande wa uongofu huwa ni ushindi mkubwa kwani kwa hatua hiyo, milango ya rehma za Mwenyezi Mungu, humfungukia mja huyo aliyefanya toba na kuazimia kutorejea dhambi ile. Aidha tulieleza kwamba, baadhi ya watu wanadhani toba au kutubia dhambi ni kutamka tu kwa ulimi. Mfanya toba anapaswa kujutia dhambi kwa moyo na kisha baada ya hapo aendeleze kwa wengine na kwa nafsi yake nara ya kuacha dhambi. Hatua inayofuata ni kuvifanya viungo vya mwili kutenda amali njema baada ya kuwa vimefanya dhambi. Na hatua ya tatu ni kuhakikisha kwamba, harejei tena kutenda dhambi. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 134 ya mfululizo huu kitazungumzia madhui ya ‘Kupenda Dunia na Kuiacha’. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Kwa hakika chimbuko la dhambi na kughafilika na utajo wa Mwenyezi Mungu ni kupenda dunia. Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema: Kuipenda dunia ni chimbuko la kila kosa (dhambi). Maneno haya ya Mtume SAW yana maana kwamba, chimbuko la makosa yote, mighafala na kuteleza ni kuipenda na kuikumbatia dunia. Siku moja Imam Hussein bin Ali as-Sajjad AS aliulizwa: Amali na matendo bora kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni nin? Imam akajibu kwa kusema: Hakuna amali na tendo bora mbele ya Mwenyezi Mungu baada ya maarifa ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kama kuifanyia uadui (kuichukia) dunia.

 

Hata hivyo tunapaswa kuzingatia nukta hii kwamba, madhumuni ya kuichukia dunia na kuipa mgongo ni kuipuuza ile dunia ambayo inamuweka mbali mwanadamu na malengo na matakwa yake makuu na ambayo inamvuta mwanadamu na kumfanya aache njia ya saada na ufanisi na kuelekea upande wa mashaka na matatizo.

Siku moja Bwana mmoja alikuwa akiiponda na kuilaumu dunia mbele ya Imam Ali bin Abi TwalibAS huku akionyesha kuichukia dunia na kuisema kwa ubaya mno. Imam Ali AS akaisifia dunia kwa kusema: Kwa hakika dunia ni nyumba ya ukweli kwa mwenye kuisadikisha, ni nyumba ya salama (kusalimika na dhambi) kwa aliyeifahamu, na nyumba ya kutosheka kwa mwenye kukusanya na kunufaika nayo, ni nyumba ya mawaidha (nasaha) kwa mwenye kuwaidhika nayo, ni mahala pa ibada kwa vipenzi wa Mwenyezi Mungu, ni mahala pa kuswali Malaika wa Allah, sehemu ya Wahyi wa Mwenyezi Mungu, ni mahala pa kufanyia biashara mawalii wa Mwenyezi Mungu, hivyo chumeni ndani yake rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu na kupata faida kwa ajili ya pepo, ni nani basi anayeiponda na kuiona dunia haina faida?....

 

 

Katika maneno mengine Imam Ali AS amenukuliwa akibainisha utambulisho na uhalisia wa dunia kwa kusema: Mtu ambaye ataitazama dunia kwa mtazamo wa ibra na mazingatio atakuwa ni mwenye kuona na mwenye weledi lakini mwenye kuitazama na kukodolea macho mapambo yake itampofusha.

Kwa msingi huo basi, kama mtu ataitazama dunia kwa ibra ataiona dunia kuwa ina mafunzo na mambo mengi ya ibra na mazingatio. Lakini kama mtu ataitazama dunia na kukodolea macho mapambo yake na kisha kuzama katika ladha na matamanio yake itampofusha mhusika. Kwa maneno mengine ni kuwa, dunia ni kama vile miwani anayovaa mtu ambapo lengo huwa ni aone vizuri zaidi.  Lakini endapo mtu badala ya kutumia miwani kuona vitu vizuri akaikodolea macho miwani yenyewe tu au badala ya kutumia kioo kuangalilia vitu vilivyoko pembeni akakikodolea macho kioo chenyewe tu, hataona kitu kingine. Kwa msingi huo basi kila panapozungumziwa dunia na toba na kuipenda dunia, makusudio ni katazo la kutumia vibaya dunia na si kitu kingine.

Bwana mmoja alimwambia Imam Jaafar bin Muhammad al-Swadiq AS, sisi tunaitafuta dunia na tunataka kuifikia. Imam akamuuliza:  Kile ambacho unakipata unapenda kukifanyia nini? Bwana yule akasema:  Ninataka kutatua haja na hawaiji zangu na za familia yangu, niwatembelee ndugu na jamaa zangu, niwasaidie masikini na watu wasiojiweza na kisha niende kutekeleza ibada ya Umra na Hija. Imam Swadiq AS akasema, hayo si kuitafuta dunia, bali ni kuitafuta akhera.

Kwa hakika kuipenda dunia na kuifanya kuwa ndilo lengo la mwisho, ni kitendo kisichofaa.

 

Wakati dunia inapokuwa ndilo lengo la mwisho la mwanadamu, mwanadamu akiwa na lengo la kuwa na udhibiti kamili, huwa tayari kufanya lolote, kuanzia wizi, khiyana, ufisadi, kutoa na kupokea rushwa na vitendo vingine vibaya mfano wa hivyo. Dunia ya namna hii na watu wenye mtazamo kama huu wa dunia, kwa hakika huhasirika na kutofaidika vyema na dunia hii kwa sababu wameifanya dunia kuwa ndio lengo lao la mwisho. Imam Ali AS anasema kuhusiana na dunia kama hii kwamba:

Wakazi wa dunia ni mbwa wabwekao na wanyama wa mwitu wangurumianao. Wenye nguvu huwala walio dhaifu, na wakubwa huwakandamiza wadogo. Ni kama mifugo, wengine wamefungwa na wengine hawakufungwa.

Aidha anasema; Dunia ni nyumba iliyo duni mbele ya Mola wake, hivyo, ikachanganywa halali kwa haramu yake, mema kwa maovu yake, na matamu kwa machungu yake.

Kadhalika Imam Ali AS anasema kuhusiana na dunia hii kwaba, Hakika dunia yenu machoni mwangu ni duni zaidi kuliko utumbo wa nguruwe ulio mkononi mwa mwenye ukoma, na ni hafifu zaidi kuliko jani lililo mdomoni mwa panzi.

Ndio maana katika kuwatahadharisha wanadamu na dunia na kuwataka wawe mamcho nayo Imam Ali AS anasema:

Itazame dunia kwa mtazamo wa mtawa aliyejitenga, na wala usiitazame kwa mtazamo wa ashiki aliyeikufia.

Kupitia maneno yaliyotangua ya Imam Ali AS tunafahamu kwamba, Imam Ali ameigawa dunia katika mitazamo miwili.

Mtazamo wa kwanza ni kuwa, mwanadamu anaweza kuitumia vizuri dunia kama njia na wenzo kwa ajili ya akhera. Kwa maana kwamba, akaifanya dunia kuwa ni shamba kwa ajili ya akhera na soko la kuchuma faida kwa ajili ya akhera yake.

Mtazamo wa pili ni kuiangalia dunia kwa tahadhari na kutoghafilika na kuifanya dunia kama ndio lengo kuu la mwisho, kwani kufanya hivyo ni kuhasirika na kupata hasara kutokana na kushindwa kunufaika vizuri na dunia hii.

Kwa msingi huo basi, mwanadamu hapaswi kuipenda na kuikumbubatia dunia na kuifanya kama ndilo lengo lake kuu bali anapaswa kuiba mgongo, lakini wakati huo huo huo akaitumia fursa ya kuweko kwake hapa dunia kupanda mazao ambayo atakwenda kupata mazao bora siku ya Akhera.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….