Dec 24, 2018 10:40 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 796 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 51 hadi 53 ambazo zinasema:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ

Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi. 

قَالُوا يَا وَيْلَنَا مَن بَعَثَنَا مِن مَّرْقَدِنَا ۜ ۗ هَـٰذَا مَا وَعَدَ الرَّحْمَـٰنُ وَصَدَقَ الْمُرْسَلُونَ

Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume. 

إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ

Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele Yetu. 

Katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita ilielezwa kwamba ulimwengu utafikia kikomo kwa irada ya Allah SW na wote walioko duniani watakata roho kwa ukelele mmoja tu wa mbinguni. Aya hizi zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Kwa irada ya Allah, ukelele mwingine wa mbinguni utapigwa na hapo watu wote watafufuka na kutoka ardhini. Ardhi itakuwa mithili ya mama mjamzito anayejifungua watoto waliomo tumboni mwake. Watu waliokuwa wamezikwa ardhini, huku viungo vya miili yao vikiwa vimetawanyika kwenye udongo – mithili ya matone ya manii yanayotoa mbegu zinazokua ndani ya mafuko ya uzazi ya akina mama – wataumbwa tena na kutoka wakiwa viumbe kamili. Ni wazi kwamba watu watakaosimamishwa katika uwanja wa Kiyama watajionea kwa macho yao na kusadikisha qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuwaumba tena waliokufa pamoja na ahadi yake ambayo walipewa na Mitume walipokuwa duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, maadi, yaani kufufuliwa viumbe yatakuwa ya kimwili; na watu wote watafufuliwa Siku ya Kiyama wakiwa na miili sawa na ile ya duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama ni siku ya majuto. Majuto kwa makafiri kwa kuiacha dini, na majuto kwa waumini kwa kutokithirisha kufanya mema na ya kheri. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba uwanja wa Siku ya Kiyama patakuwa pahala pa kuhudhurishwa wanadamu wa zama zote katika mahali pamoja na katika wakati mmoja.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 54 hadi 58 ambazo zinasema:

فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ

Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ

Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ

Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.

سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ

"Salam!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.

Kuhudhurishwa Siku ya Kiyama ni kwa ajili ya kusimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah ili kila mtu alipwe kulingana na fikra, imani na matendo aliyofanya duniani. Kwa muktadha huo Qur'ani tukufu inasema: Katika mahakama hiyo, kila kitu kitapimwa kwa mizani ya Mwenyezi Mungu, na hakuna mtu atakayefanyiwa hata chembe ya dhulma. Waja wema watalipwa malipo mema ya thawabu na wale wabaya mwisho wao utakuwa wa adhabu na iqabu. Kisha aya zinasimulia hali za watu wa Peponi na kutaja baadhi ya neema za huko ambazo zinaweza kutasawarika na kufahamika kwa wakazi wa duniani. Neema hizo ni za aina ya vyakula, mavazi, maskani na wake, ambazo ni vielelezo vya hali ya raha na utulivu. Hizo ni neema zitakazoendana na irada na matakwa ya waja wenyewe wa Peponi. Watapata humo kila watakachotamani na kitakachowaburudisha, pasi na kuwachosha wala kuwakinaisha. Tab'an mbali na neema za kimaada, waja wa Peponi watapata pia neema maalumu za kimaanawi. Maamkizi ya salama na amani yatokayo kwa Mola ambayo ni ishara ya rehma makhsusi za Allah kwa watu wa Peponi yatawapa utulivu na ukunjufu ulio bora waja hao kuliko neema yoyote ile ya kimaada. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya kudhihiri na kushuhudiwa uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; na kila mtu atapata malipo ya amali zake bila kujali mafungamano na nasaba aliyokuwa nayo duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Peponi ni mahali pa raha na furaha tupu, pasipo na aina yoyote ya majonzi wala chembe ya huzuni. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hata Peponi pia watu wataishi kifamilia; na wanandoa watakuwa wakistareheshana. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba huko Peponi hakutakuwa na mpaka wa aina yoyote kwa mtu, bali chochote kile kizuri atakachokitaka na kukitamani mtu, atakipata. Allah atujaalie kwa rehma zake kuwa miongoni mwa watu wa Peponi, amin. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 796 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

Tags