Dec 24, 2018 10:49 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 797 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 59 ambayo inasema:

وَامْتَازُوا الْيَوْمَ أَيُّهَا الْمُجْرِمُونَ

Na jitengeni leo enyi wakosefu!

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea nafasi na makazi ya watu wa Peponi ambayo yatawafanya waja hao wema wapate raha ya kimwili na utulivu wa kiroho na akili. Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Siku hiyo safu za watu wabaya na watu wema zitatenganishwa, kwa wabaya hao kuelekezwa kwenye njia nyingine ambayo inaishia kwenye adhabu ya Moto wa Jahannamu wenye machungu na mateso makali. Watu hao walikhitari na kufadhilisha raha na starehe za kupita za dunia kuliko neema za milele za akhera na kwa hivyo wataishia kwenye adhabu ya milele ya Moto. Bila shaka malipo hayo yatakuwa ni matunda ya uchaguaji waliofanya wao wenyewe wa kufuata njia potofu. Na kwa kuwa Siku ya Kiyama itakuwa ya Mahakama ya kutekelezwa uadilifu wa Allah, haitakuwa na maana kwa wema na wabaya kuwekwa katika safu moja kama walivyokuwa wakiishi na kuchanganyika pamoja katika maisha ya duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya kutenganika watu kulingana na fikra, itikadi na amali zao. Siku hiyo si hasha wazazi wakatengana na watoto wao, na si hasha watu wasio na ujamaa wowote wakawa wako pamoja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Siku ya Kiyama ni siku ya kuthibiti ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwalipa thawabu waja waliotenda mema na kuwapa adhabu wale waliotenda mabaya.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 60, 61 na 62 ambazo zinasema:

أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.

وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ

Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

وَلَقَدْ أَضَلَّ مِنكُمْ جِبِلًّا كَثِيرًا ۖ أَفَلَمْ تَكُونُوا تَعْقِلُونَ

Na hakika yeye amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?

Aya hizi zinawahutubu waovu na wafanya madhambi waliohudhurishwa kwenye uwanja wa Siku ya Kiyama huku safu zao zikiwa zimetenganishwa na zile za waumini. Kusemeshwa watu hao na Allah kutaambatana na kemeo na karipio, kwamba, kwa nini mlimfuata na kumtii shetani na kuipuuza njia ya Mola wenu? Qur'ani tukufu inalielezea tamko hilo la Allah SW kama ukumbusho wa ahadi ambayo Yeye Mola aliichukua kwa watu wote mwanzoni mwa kuumbwa kiumbe mwanadamu. Wakati Nabii Adam na mkewe Hawa walipohadaiwa na hila za shetani peponi, Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwatanabahisha kwa kuwauliza, ilikuwaje mkaathiriwa na wasiwasi wa shetani mpaka mkakila kitu ambacho nilikukatazeni kukila? Kwani hamjui kama shetani ni adui yenu? Kulingana na fitra aliyojaaliwa na Mola, mwanadamu anajua kama kufanya maovu hakuendani na utu wake; na mtu yeyote yule, na kwa sababu yoyote ile, anayemshawishi mwenzake kufanya maovu, huyo ni shetani; awe ni wa jinsi ya binadamu au la. Fitra na maumbile aliyojaaliwa na Mola yanamkataza mtu kufanya mabaya na kumshajiisha kutii amri za Mola wake Muumba. Lakini mbali na fitra na maumbile ya batini, tunapoiangalia hali na mazingira ya nje katika historia za kaumu zilizopita pia tunabaini kuwa watu wengi walighariki kwenye dimbwi la madhambi na maovu; na hatima yao ikawa ni kuishia kwenye dhalala, upotofu na maangamizi. Kama tutayachunguza maisha ya watu wa aina hiyo tutabaini kuwa sababu ya kupotoka kwao ilikuwa ni kufuata mambo ya khurafa na kuwatii watu waliopotoka na wenye fikra potofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kwa mwanadamu kupitia fitra na akili ya batini aliyompa pamoja na Mitume aliompelekea kwamba hatoifuata katu njia ya shetani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mtu hawezi kujivua na moja kati ya hali mbili. Ama ya kuwa mtumwa wa Allah au ya kuwa mtumwa wa Shetani. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, katika kila Sala tunayosali tunamwomba Allah atuongoze njia iliyonyooka. Kwa mujibu wa aya hizi njia iliyonyooka ni ya kumtii na kumwabudu Yeye Mola. Vilevile aya hizi zinatutaka tusiwe tunatafakari na kutumia akili katika masuala ya ustawi wa maisha tu lakini pia tuitumie kutalii historia za waliotangulia na kupata ibra na mazingatio ya hatima na mwisho mbaya wa wale waliohadaiwa na kughilibiwa na shetani.   

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 63 hadi 65 ambazo zinasema:

هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ

Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.

اصْلَوْهَا الْيَوْمَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ

Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. 

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme Nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia katika kuzungumzia hali ya watu waovu Siku ya Kiyama kwa kueleza kwamba: Mitume waliwafikishia watu duniani ahadi ya Allah SW ya wafanyao mema kulipwa thawabu na wale watendao maovu kulipwa adhabu, lakini akthari ya watu hawakuiamini ahadi hiyo na wakawa wanaifanyia shere na stihzai. Lakini leo wanashuhudia kwa macho yao kuthibiti kwa ahadi hiyo katika uwanja wa Siku ya Kiyama. Na si watauona tu Moto, bali watauingia na kuuhisi muunguzo wake kwa ujudi wao wote. Katika mahakama hiyo ya uadilifu ya Allah hakutakuwepo na haja ya kuwataka watu waovu waseme chochote kile ili kuficha au kukana waliyoyafanya duniani, kwa sababu badala ya ulimi, mikono na miguu pamoja na viungo vyao vyengine vitawezeshwa kusema na kubainisha yote waliyoyatenda. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume waliwatimizia watu wote dhima ya kuwafikishia wito wa haki na kuwatahadharisha kila mara na adhabu ya Moto. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama, mdomo ambao ni kiungo cha kusemea utafungwa na badala yake mikono na miguu ndiyo itakayonena. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba viungo vya mwili wa mwanadamu vina aina maalumu ya umaizi na utambuzi; na kwa hiyo vinayarekodi na kuyahifadhi yote yanayojiri mbele yao na vitakwenda kuyabainisha Siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 797 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale watakaofuzu na kuingizwa Peponi Siku ya Kiyama na si katika wale watakaohasirika kwa kuselelea Motoni. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags