Jumanne 25 Disemba 2018
Leo ni Jumanne tarehe 17 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na tarehe 25 Disemba 2018.
Siku kama ya leo miaka 2019 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa. Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wafuasi wa kweli wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu

Miaka 375 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi.
Miaka 353 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 25 Disemba 1665, Ufaransa ilianzisha French East India Company katika kipindi cha utawala wa Mfalme Louis II ili kushindana kisiasa, kiuchumi na kikoloni na serikali ya Uingereza huko India. Uingereza ilikuwa imeasisi British East India Company miaka 66 kabla ya hapo. Vilitokea vita kadhaa baina ya tawala hizo mbili za kikoloni kwa shabaha ya kuikoloni ardhi ya India.

Miaka 142 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Muhammad Ali Janah, mpigania uhuru mashuhuri wa Bara Hundi na mwasisi wa Pakistan. Janah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Janah alikuwa miongoni mwa shakhsiya wakuu walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita aliaga dunia msomi mkubwa wa hadithi Mullah Muhammad Nakhjawani. Mullah Nakhjawani alibobea sana katika elimu za fiqhi na hadithi na lifuatwa zaidi na Waislamu wa eneo la Kaukazia. Ayatullah Nakhjawani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 katika mji mtakatifu wa Karbala na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa.

Tarehe 25 Disemba miaka 41 iliyopita alifariki dunia msanii mashuhuri na mcheza filamu za kuchekesha Charlie Chaplin. Sir Charles Chaplin anatambuliwa kuwa mtayarishaji, mchezaji na mtengeneza filamu mkubwa wa Holywood na mshindi wa tuzo ya Oscar. Filamu nyingi za msanii huyo ni za vichekesho na za kimyakimya zisizo na sauti. Alifanya kazi katika tasnia ya filamu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 65 na alianza kazi hiyo katika ukumbi wa Victoria nchini Uingereza akiwa mtoto hadi alipokamilisha umri wa miaka 88. Mwaka 1919 Charles Chaplin na wenzake kadhaa walianzisha Jumuiya ya Filamu. Msanii huyo mashuhuri alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na maradhi ya kisukari.
Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1979, viongozi watatu wa ngazi za juu wa Palestina waliuawa kigaidi na Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Viongozi hao walikuwa Ali Hassan Salamah, afisa wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliyeuawa Beirut baada ya kutegwa bomu ndani ya gari lake, Samir Touqan mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya PLO huko Cyprus na Ali Nasser Yassin, shakhsia mwingine wa Palestina aliyekuwa mwakilishi wa PLO nchini Kuwait. Jinai hiyo ilidhihirisha tena jinsi utawala katili wa Israel unavyotumia ugaidi katika maeneo mbalimbali dunia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu.