Jan 02, 2019 08:20 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 808, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 50 hadi 53 ambazo zinasema:

فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ

Tena wataelekeana wao kwa wao wakiulizana.

قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ إِنِّي كَانَ لِي قَرِينٌ

Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nilikuwa na rafiki.

يَقُولُ أَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُصَدِّقِينَ

Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki? 

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَدِينُونَ

Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, (tutafufuliwa) na kulipwa?

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa watu wa peponi watakaa juu ya viti huku wakiburudika kwa raha za peponi kwenye dhifa za mijumuiko na mazungumzo ya upendo na masahibu zao. Aya tulizosoma zinasimulia kuhusu moja ya mazungumzo yatakayojiri baina ya watu wa peponi ili yazingatiwe na kuwa ukumbusho kwa sisi tulioghafilika,  kwa kutufanya tuelewe kwamba si hasha watu wakawa marafiki na masahibu wasiobandukana hapa duniani lakini Siku ya Kiyama wataachana mkono kwa mmoja kuelekea peponi na mwengine kuishia motoni! Kwa mujibu wa aya hizi, katika mazungumzo yao, watu wa peponi watakuwa wanaulizana kuhusu mambo yaliyowatokezea duniani na kila mmoja atasimulia kumbukumbu yake. Mmoja wao atahadithia kumbukumbu ya rafiki yake wa duniani aliyekuwa akikanusha Kiyama na kudhani kwamba kuwa hai tena watu baada ya kufa ni jambo muhali na lisilowezekana. Mtu huyo alikuwa akimuuliza kwa mshangao sahibu yake huyo muumini: Hivi kweli wewe unaamini jambo hili? Ni kweli unaitakidi kwamba tunayoyafanya duniani yatalipwa malipo ya thawabu na adhabu baada ya ulimwengu huu? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kusuhubiana na watu wasioshika dini au wenye imani dhaifu hakukatazwi, ikiwa hakutasababisha kudhoofika imani na itikadi ya mtu; hasa kama ataweza kuwalingania na kuwavuta watu hao kwenye dini na njia ya haki au angalau kuyapatia jawabu masuali yao ya kifikra. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wakadhibishaji wa maadi, yaani kufufuliwa viumbe hawana hoja ya kimantiki wala ya kijarabati ya kupingia hilo na kuwepo kwa ulimwengu mwingine baada ya kifo. Kitu pekee wanachofanya ni kustaajabia na kuliona jambo hilo kuwa ni baidi kutokea. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Siku ya Kiyama kumbukumbu za mtu za hapa duniani hazitasahaulika; kwani ataweza kuyakumbuka yaliyomtokezea maishani mwake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 54 hadi 57 ambazo zinasema:

قَالَ هَلْ أَنتُم مُّطَّلِعُونَ

Atasema: Je! Nyie mnataka kujua hali zao?

فَاطَّلَعَ فَرَآهُ فِي سَوَاءِ الْجَحِيمِ

Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. 

قَالَ تَاللَّـهِ إِن كِدتَّ لَتُرْدِينِ

Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza.

وَلَوْلَا نِعْمَةُ رَبِّي لَكُنتُ مِنَ الْمُحْضَرِينَ

Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa (motoni).

Yule mja wa peponi ataendelea kuhadithia kumbukumbu zake kwa masahibu zake wa peponi kwa kusema: yule mtu ambaye tulipokuwa duniani alikuwa akitilia shaka na kunipinga kwa sababu ya imani yangu juu ya Kiyama, leo anaadhibika motoni. Kama mtataka, mnaweza kuona hali aliyonayo motoni. Tab'an kutokana na kusuhubiana naye na kuwa na urafiki naye, mimi pia ilikuwa nusura niteleze na kupotoka; na pengine si hasha leo ningekuwa pamoja naye motoni, lakini Mwenyezi Mungu amenirehemu na kuniokoa na hilaki na maangamizi haya kutokana na imani yangu na amali njema alizonipa taufiki ya kuzifanya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa mujibu wa aya za Qur'ani watu wa peponi watakuwa wanajua kinachoendelea kwa watu wa motoni, na wakati wowote ule watakapotaka wataweza kujua watu hao wako kwenye hali gani na kuweza kuzungumza nao; lakini watu wa motoni hawatoweza kuwaona watu wa peponi na kuelewa hali walizonazo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kusuhubiana na kuwa na urafiki na wakadhibishaji wa dini hakuna mushkili ikiwa hakutakuwa sababu ya kudhoofika imani ya mtu. Pamoja na hayo kuwa na urafiki na watu wa aina hiyo ni hatari; na kama si rehma na hifadhi ya Allah mtu anaweza kuathiriwa nao na kuishia motoni kama wao.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 58 hadi 61 ambazo zinasema:

أَفَمَا نَحْنُ بِمَيِّتِينَ

Je! Sisi hatutakufa, 

إِلَّا مَوْتَتَنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ

Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa?

إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa.

لِمِثْلِ هَـٰذَا فَلْيَعْمَلِ الْعَامِلُونَ

 Kwa mfano wa haya nawatende watendao. 

Ni dhahiri kwamba mtu atakayeingia peponi atajua kuwa hatofikwa na adhabu, kwa sababu kama ingebidi aadhibiwe lingempata hilo kabla ya kuingia peponi. Lakini kuzungumziwa nukta hii katika aya hizi na kubainishwa kwa ulimi kumefanyika kwa sababu mbili: Moja ni kukumbusha kuhusu uraufu na ukarimu wa Mola ambao unamfanya mja awe mshukurivu kwake. Lakini sababu nyingine ya kulitaja hilo, ambayo ni daraja ya juu kabisa ya neema kwa mtu, ni kwamba huko akhera ataishi peponi milele pasi na kusibiwa na maradhi yoyote wala kuzeeka, mambo ambayo yalikuwa sababu ya yeye kufikwa na mauti duniani. Tukumbuke pia kwamba umri wa duniani ni mfupi na uliojaa misukosuko, tabu, machungu na mateso, lakini maisha ya akhera hayana mwisho; na watu wa peponi watakuwa kwenye raha, starehe na neema za milele. Aya ya mwisho tuliyosoma inabainisha ujumbe wa watu wa peponi kwa walimwengu, nao ni kwamba: enyi watu ambao mngali na fursa ya kuishi duniani mkiwa na bakio la umri, jitahidini kadiri muwezavyo kufanya mema na ya heri ili muweze kujiwekea akiba na masurufu mengi zaidi kwa ajili ya safari ya akhera. Mali na utajiri ni bidhaa zenye thamani kwa matumizi ya duniani, lakini katika soko la akhera bidhaa inayonunuliwa ni amali tu za mtu; na kila mtu atapimwa kwa amali zake, si kwa mali na utajiri, wala madaraka, hadhi na umaarufu wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba peponi hakuna kifo wala kutoweka; lakini motoni, waovu watakuwa wakikata roho kwa mateso ya adhabu na kisha kufufuliwa tena. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa saada na kufuzu kwa kweli kunapatikana kwa mtu kujichunga asije akateleza na kupotoka katika mazingira maovu, ili aweze kufika alikokusudiwa akiwa safi na salama. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mambo anayoyafanya mtu hapa duniani inapasa yawe kwa ajili ya kufikia malengo aali na uokovu wa kweli, la sivyo mwanadamu atafikwa na majuto na hasara kubwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 808 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags