Jan 02, 2019 08:32 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 809, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 62 na 63 ambazo zinasema:

أَذَٰلِكَ خَيْرٌ نُّزُلًا أَمْ شَجَرَةُ الزَّقُّومِ

Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum?

إِنَّا جَعَلْنَاهَا فِتْنَةً لِّلظَّالِمِينَ

Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso na adhabu kwa walio dhulumu.

Katika darsa iliyopita tuliashiria baadhi tu ya neema za peponi na raha na starehe watakazokuwa nazo watu wa peponi. Zikiendeleza maudhui hiyo, aya tulizosoma zinalinganisha hali yao hiyo na hali ya watu wa motoni kwa kuhoji: Kukirimiwa na kuhudumiwa watu wa peponi kwa anuai za vinywaji vya kuburudisha ni bora au watakavyofanyiwa watu wa motoni kwa kufakamizwa vilaji na vinywaji vichungu na vya kukirihisha? Ni wazi kwamba mawili haya hayawezi kufananishwa mpaka ihojiwe ni lipi bora zaidi. Kwa sababu motoni si mahali pa raha na starehe hata tupalinganishe na peponi kulikojaa anuai za vitu vyenye raha na ladha tamu. Kwa hivyo ulinganishaji wa aina hii umefanywa ili uwe ukumbusho na tanabahisho kwa watu walioghafilika, kwamba kama mnahisi mnaburudika na kustarehe kwa matendo yenu maovu mnayofanya duniani yalinganisheni hayo na raha na starehe za milele za peponi na adhabu na mateso mtakayopata motoni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika kulinganisha mambo haya na yale tunayofanya tusiishie kuangalia matokeo na athari zake za muda tu na za kupita za duniani, lakini tufikirie pia thawabu na adhabu zake za akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dhulma ndicho kipimo cha kumfanya mtu aingizwe motoni. Kuifanyia dhulma mtu nafsi yake na wenzake na kuifanya dhulma dini, Allah na mawalii wa Allah.       

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 64 hadi 66 ambazo zinasema:

إِنَّهَا شَجَرَةٌ تَخْرُجُ فِي أَصْلِ الْجَحِيمِ

Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu.

طَلْعُهَا كَأَنَّهُ رُءُوسُ الشَّيَاطِينِ

Mashada ya matunda yake kama kwamba ni vichwa vya mashet'ani.

 فَإِنَّهُمْ لَآكِلُونَ مِنْهَا فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ

Basi hakika hao bila ya shaka watakula katika huo, na wajaze matumbo kwa huo.

Aya hizi zinaelezea kuhusu Zaqqum, kama ambavyo maelezo yanayofanana na hayo yamekuja pia katika aya ya 43 hadi 46 za Suratu-Dhukhan. Kwa mujibu wa majimui ya aya za sura mbili hizi, zaqqum ni aina ya mmea na mti unaoota ndani ya Moto unaohilikisha wa Jahannamu; na watu wa motoni watakuwa wakila matunda yatokanayo na mti huo. Ni wazi kwamba mmea unaoota na kumea kwa moto badala ya maji una hali maalumu ya muunguzo; na matunda yake humletea adhabu na mateso mwenye kuyala. Lakini mbali na harufu mbaya ya uvundo na ladha mbaya ya matunda ya mti huo, Qur'ani tukufu imeushabihisha katika ubaya na kutisha kwake na kichwa cha zimwi au shetani. Inafaa kuashiria kuwa tokea hapo kale watu walikuwa wakikielezea kichwa cha zimwi kama kitu kinachotisha, kama ambavyo taswira waliyokuwa wameijenga akilini mwao kuhusu malaika ilikuwa ya kiumbe jamili na mwenye kupendeza, ilhali hakuna yeyote kati yao aliyewahi kumwona zimwi au malaika! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mfumo wa akhera ni tofauti kabisa na mfumo wa duniani. Kwa hivyo upo uwezekano wa kuota mmea na miti kwenye miale ya moto na kando ya watu wanaoteketea motoni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wale ambao duniani walikuwa wakimtii shetani, huko motoni akhera watakumbana na mimea ambayo badala ya mandhari nzuri na za kuvutia za kijani kibichi itakuwa na mandhari mbaya na za kuchukiza utadhani ni vichwa vya kutisha vya mazimwi na mashetani vimeota na kumea kutoka ardhini.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 67 na 68 ambazo zinasema:

ثُمَّ إِنَّ لَهُمْ عَلَيْهَا لَشَوْبًا مِّنْ حَمِيمٍ

Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.

ثُمَّ إِنَّ مَرْجِعَهُمْ لَإِلَى الْجَحِيمِ

Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.

Bila shaka kula matunda ya Zaqqum kutasababisha kiu tu kwa mtu na kwa hivyo aya tulizosoma zinasema: wale watakaokula matunda ya mti wa Zaqqum watakunywa maji kwa ajili kuondoa kiu waliyonayo; lakini maji hayo yatakuwa makali mno, machafu na yenye kuunguza, ambapo badala ya kuondoa kiu yataifanya iwe kali zaidi. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: baada ya hatua hizo, watu hao wataingizwa rasmi motoni. Kwa hivyo yale yaliyozungumziwa kuhusu mti wa Zaqqum na kinywaji baada yake ni kuhusu mambo watakayofanyiwa watu wa motoni kabla ya kuingizwa kwenye moto. Ni kama wanavyohudumiwa wageni wakati wanapoanza kuwasili kwenye hadhara na hafla ya sherehe na burudani. Sasa kama kuhudumiwa kwa waovu kabla ya kuingia kwenye moto wa Jahannamu kuko hivyo, watafanyiwa yepi watakapoingia motoni kwenyewe? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watu wa motoni watakuwa na vilaji na vinywaji kama watu wa peponi, lakini vilaji na vinywaji hivyo si tu havitakuwa na ladha tamu na ya kuburudisha lakini pia vitakuwa na sura mbaya na ya kuchukiza ya kuwafanya wakirihike na kuadhibika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wale wanaoyajaza matumbo yao vya haramu hapa duniani bila kujali maamrisho na makatazo ya Allah Siku ya Kiyama pia matumbo yao yatajazwa vitu vitakavyowatesa na kuwaadhibu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Kiyama kitakuwa na mapito na vituo tofauti. Baada ya watu wa motoni kuzipita awamu tofauti, hatimaye wataingizwa kwenye makazi yao makuu na ya asili ya motoni. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 809 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema, duniani na akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags