Jan 05, 2019 09:20 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 819, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 149 hadi 152 ambazo zinasema:

فَاسْتَفْتِهِمْ أَلِرَبِّكَ الْبَنَاتُ وَلَهُمُ الْبَنُونَ

Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wana watoto wa kiume?

أَمْ خَلَقْنَا الْمَلَائِكَةَ إِنَاثًا وَهُمْ شَاهِدُونَ

Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?

 أَلَا إِنَّهُم مِّنْ إِفْكِهِمْ لَيَقُولُونَ

Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:

وَلَدَ اللَّـهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ

Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo! 

Hadi kufikia hapa, sura hii ya Ass 'Affat imezungumzia habari za Mitume kadhaa wa Allah na kaumu zao. Aya hizi tatu tulizosoma zinaashiria imani potofu za washirikina wa Makka na kueleza kwamba: Wao walikuwa wakimtasawari Mwenyezi Mungu sawa na alivyo mwanadamu, kwamba ana watoto, na malaika ni mabinti zake; na namna hivyo wakawa wanamlinganisha Allah na viumbe wake. Aya hizi zinapinga imani hizo potofu na kuwaambia watu hao: Nyinyi washirikina mnawachukia watoto wa kike na kuwaona kuwa ni nuhusi, kiasi kwamba kama mngaliweza mngewazika mabinti zenu wakiwa hai. Sasa inakuwaje mnapotaka kumnasibishia Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto mnafanya hivyo kwa watoto wa kike na nyinyi wenyewe mnajinasibishia watoto wa kiume? Hapana shaka kuwa mtoto wa kike na wa kiume wana hali sawa mbele ya Mwenyezi Mungu, wala kati yao, hakuna aliye kwa dhati yake mbora kuliko mwenzake. Lakini hapa Qur'ani tukufu inajadiliana na washirikiana kwa kutumia mantiki wanayoikubali wao wenyewe. Kisha aya zinaendeleza mjadala huo kwa kuwahoji: Je, haya mnayodai yana hoja na ushahidi wowote? Wakati malaika walipoumbwa, je nyinyi mlikuwepo na mlishuhudia kuumbwa kwao, mkajua kama jinsia yao ni ya kike? Kwa nini mnayanasibisha na Mwenyezi Mungu mambo yasiyostahiki kwa kutegemea mawazo na dhana tu? Kwani Yeye Allah hasa ana mwana, hata mnaleta mjadala wa mwana huyo kama ni mwanamke au mwanamme? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume walijaribu kutumia mbinu ya kuwauliza masuali washirikina na wakanushaji haki, ili watafakari na kutanabahi kwamba imani na itikadi walizonazo sio sahihi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kinyume na picha za michoro zilizoenea miongoni mwa wafuasi wa baadhi ya dini, zinazotoa taswira ya malaika kama viumbe wenye sura na maumbo ya kike, kwa mujibu wa aya za Qur'ani, imani na dhana hiyo ni potofu na ya kishirikina, na wala haiendani na mafundisho ya Kitabu hicho cha mbinguni.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 153 hadi 157 ambazo zinasema:

أَصْطَفَى الْبَنَاتِ عَلَى الْبَنِينَ

Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? 

مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?

أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

Hamkumbuki?

أَمْ لَكُمْ سُلْطَانٌ مُّبِينٌ

Au mnayo hoja iliyo wazi? 

فَأْتُوا بِكِتَابِكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuwahoji tena washirikina kwamba: Inakuwaje nyinyi mnawafikiria Malaika kuwa ni mabinti na kuwanasibisha na Mwenyezi Mungu? Mnadhani Mwenyezi Mungu amemfanya mtoto wa kike kuwa bora kuliko mtoto wa kiume na kwa hivyo hakujichagulia mtoto wa kiume? Haujafika wakati wa nyinyi kuzinduka na kuacha khurafa hizo na maneno hayo yasiyo na msingi wala maana yoyote? Kutafakari kidogo tu juu ya suala hili kunatosha kuweka wazi ubatilifu wa imani hiyo; wala haihitaji kuwaza na kutafakari kwa kina. Baada ya Qur'ani tukufu kuzivunja kwa njia ya mantiki hoja na imani potofu za washirikina kuhusu Malaika inasema: Kama katika vitabu vilivyotangulia pia mnao ushahidi wa maandiko unaothibitisha madai yenu uleteni pia. Kwenye kitabu au andiko gani la mbinguni litokalo kwa Mwenyezi Mungu au Mitume wake linalothibitisha kuwa Allah SW ana mwana, na malaika ni watoto wake?! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu ambao, kwa mtazamo wao mtoto wa kike ni mbaya na mtoto wa kiume ndiye mzuri na wanawanasibisha watoto wa kike na Mwenyezi Mungu na watoto wa kiume na wao wenyewe, wana itikadi batili na potofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, itikadi na imani za mtu kuhusu Mwenyezi Mungu inapasa zitokane na hoja za mantiki au za maandiko. Haiwezekani kumnasibishia kitu Allah SW kwa kutegemea mawazo na dhana batili.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 158 hadi 160 ambazo zinasema:

وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ۚ وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ

Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa.

سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ

Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia.

 إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ

Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio takaswa.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia imani potofu za washirikina kuhusu malaika, aya hizi zinasema: Wao walikuwa wakiitakidi pia kuwepo uhusiano na nasaba baina ya Mwenyezi Mungu na majini. Baadhi ya washirikina wakiitakidi kwamba, jini ni mke wa Mungu na baadhi yao wakiwaitakidi majini kwamba wana aina fulani ya ushirika na Mwenyezi Mungu na hata wakawa wanawaabudu. Lakini Qur'ani tukufu inaipinga na kuikemea vikali imani hiyo ya khurafa na uzushi na kueleza kwamba: Vipi majini wanaweza kuwa na hadhi kama hiyo mbele ya Allah SW ilhali Siku ya Kiyama wao majini watawajibishwa, kwa kutakiwa wajieleze kwa waliyoyafanya na kuhudhurishwa mbele ya mahakama ya Mola ili kulipwa thawabu au adhabu kwa matendo yao? Katika sehemu ya mwisho ya aya tulizosoma, ambazo zinakana na kupinga imani potofu za washirikina kuhusu Mwenyezi Mungu, Qur'ani tukufu inasema: Allah SW ametakasika na haya yote anayonasibishwa nayo; na hakuna yeyote ghairi ya Mitume na mawalii wa Allah waliotakaswa na kila aina ya shirki na uchafu, awezaye kumuelezea na kumzungumzia kwa usahihi Yeye Mola aliyetukuka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ikiwa mwanadamu atatoka nje ya mipaka ya akili na mantiki yamkini akanasibisha kwa Mwenyezi Mungu na kwa masuala ya dini kila aina ya khurafa na kauli zisizofaa, na hata kufikia kiwango cha upotofu cha kumuitakidi jini kuwa mke wa Mwenyezi Mungu! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, jini ni kiumbe halisi, ambaye kama alivyo mwanadamu ana akili na ana majukumu; na Siku ya Kiyama atahudhurishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah ili kuhesabiwa kwa amali zake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 819 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na imani potofu zikiwemo za kumnasibisha Yeye na mambo yasiyostahiki. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags