Jan 21, 2019 01:37 UTC
  • Jumatatu tarehe 21 Januari 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 14 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na tarehe 21 Januari 2019.

Siku kama ya leo miaka 40 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, milango ya jela za utawala wa Shah ilifunguliwa na wananchi Waislamu wa Iran wakawaachia huru watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosema: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Sijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, Vladimir Ilyich Lenin, kiongozi wa mapinduzi ya kikomonisti ya Umoja wa Kisovieti alifariki dunia. Lenin alizaliwa mwaka 1870. Alianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa kifalme wa Russia tangu akiwa Chuo Kikuu. Kutokana na harakati zake hizo, mara kadhaa Lenin alifungwa jela na kubaidishwa. Katika kipindi cha kuwa kwake jela, Lenin aliandika vitabu kadhaa.

Vladimir Ilyich Lenin

Katika siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, Mfalme Louis XVI wa Ufaransa anayejulikana pia kama Louis Capet. alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi nchini Ufaransa mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe yaani Malkia Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XVI kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa Mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XVI akiwemo mkewe Marie-Antoinette nao pia walitiwa kitanzi.

Mfalme Louis XVI

Miaka 282 iliyopita yaani tarehe 21 Januari 1723, tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo. Ghuba ya Bengali iko kaskazini mashariki mwa Bahari ya Hindi na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali za watu.

Kimbunga kikali

 

Tags