Jan 24, 2019 04:05 UTC
  • Alkhamisi tarehe 24 Januari 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa 24 Januari 2019.

Siku kama hii ya leo miaka 40 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapour Bakhtiar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kuwasili hapa nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni huko Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran.

Shapour Bakhtiar

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika Bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Winston Churchill

Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani. Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

Kisima cha kwanza kabisa cha mafuta duniani

Siku kama ya leo miaka 352 iliyopita, Mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.

Mkataba wa Breda kati ya Uingereza na Uholanzi

Na miaka 990 aliyopita mwakafa na siku kama ya leo, alizaliwa mwanafalsafa na msomi mkubwa wa Kiislamu na Kiirani Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo akiwa na umri wa miaka 28. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khawaja Nidham al-Mulk kumualika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea kwake Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani viitwavyo "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."

Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi

 

Tags