Jan 28, 2019 07:26 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 28

Hujambo mpenzi msikilizaji wa na haswa mpenzi na mfuatiliaji wa spoti, na karibu tuangazie baadhi ya matukio ya michezo ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa...

Kombe la Asia: Iran yatinga nusu fainali

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutinga nusu fainali katika michuano ya Kombe la Asia. Hii ni baada ya kuibamiza China mabao 3-0 katika mchuano huo wa kusisimua uliopigwa Alkhamisi katika Uwanja wa Mohammed bin Zayed mjini Abu Dhabi, Iran iliwanyoa bila maji vijana wa Kichina na hivyo kujikatia tiketi ya kucheza nusu fainali. Bao la kwanza la Iran lilitiwa wavuni na Mehdi Taremi baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Sardar Azmoun, dakika 18 baada ya kuanza ngoma.

Team Melli ikipambana na China

Katika dakika 30 ya mchezo, Azmoun naye alipachika kimyani bao la pili lililomuacha taabani kipa wa China, Yan Junling. Mtoka benchi, Karim Ansarifard alifanya mambo kuwa 3-0 kutokana na uzembe wa mabeki wa China.

Japan ambayo inacheza na Iran Jumatatu ilifanikiwa kuingia nusu fainali hiyo baada ya kuitoa Vietnam kwa bao 1-0 katika mchezo wa robofainali. Iran imeshinda taji hilo mara 3, mara ya mwisho ikilitwaa kombe hilo zaidi ya miongo mitatu iliyopita. Qatar itashuka dimbani kuvaana na Imarati katika mchuano mwingine wa nusu fainali Jumanne hii, ambapo mshindi atajikatia tiketi ya kucheza fainali.

Karate: Iran medali lukuki Paris

Makarateka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali sita katika Mashindano ya Ligi Kuu ya Karate 1 yaliyofunga pazia lake Jumapili katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Makarateka wa Iran ya Kiislamu

Wanakarate hao wa Kiirani wamezoa medali moja ya dhahabu, fedha tatu na shaba mbili katika mashindano hayo ya siku mbili. Makarateka 776 kutoka nchi 82 duniani wameshiriki mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Karate Duniani WKF, na waliofuzu watashiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka ujao 2020.

Kombe la Sportpesa

Klabu ya Kariobangi Sharks ya Kenya imetwaa Kombe la SportPesa mwaka huu baada ya kuichachafya timu nyingine ya nchi iyo, klabu ya Bandari katika kitimutimu cha fainali kilichofanyika Jumapili. Kikosi cha Kariobangi cha jijini Nairobi kimetwaa ubingwa baada ya kuwafunga Wapwani goli moja bila jibu katika fainali hiyo ya kukata na shoka iliyopigwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam nchini Tanzania. Bao hilo la kipekee la mechi na la ushindi kwa Kariobangi Sharks lilifungwa na Harrison Mwendwa.

Kinara wa upinzani Kenya, Raila Odinga akiwakabidhi Kombe wachezaji wa Kariobangi Sharks

Mshindi wa Kombe la SportPesa mbali na kuzawadiwa dola elfu 30, lakini pia watapata fursa adimu ya kuvaana na klabu ya Everton ya Ligi Kuu ya soka ya Uingereza. Wakati huohuo, klabu ya Simba ilikabiliana na Mbao FC zote za Tanzania kutafuta mshindi wa tatu. Simba baada ya lalama kutoka kwa mashabiki hawakuwa na budi kunyakua nafasi ya 3 japo kwa mbinde. Baada ya kulazimishwa sare tasa na Mbao FC, timu hizo zililazimika kukabiliana katika upigaji penati, ambapo Simba ilishinda kwa magoli 5-3.

Simba ambao msimu uliopita walipoteza katika fainali ya michuano hiyo dhidi ya Gor Mahia, safari hii imeshindikana kurudia rekodi yao na wamejikuta wakitolewa katika hatua ya nusu fainali kwa kufungwa kwa magoli 2-1 dhidi ya klabu ya Bandari FC ya Kenya, na ndipo wakaishia kucheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.  Timu za Tanzania hazijawahi kutwaa taji hilo toka lianzishwe miaka mitatu iliyopita. Mabingwa watetezi wa taji hilo la SportPesa, Gor Mahia ya Kenya, waliondolewa katika michuano hiyo, baada ya kufungwa na Mbao FC ya Tanzania kwa mabao 4-3 katika mechi ya muondoano, kupitia mikwaju ya penalti.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeiondoa klabu ya Ismaily ya Misri kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi. CAF imeiandikia klabu hiyo barua kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu na kurusha mawe na chupa za maji uwanjani wakati wa mechi namba 96 ambapo timu hiyo ilikuatana na klabu Africa ya Tunisia Januari 18 mwaka huu mjini Ismailia Misri. Mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kumaliza mechi dakika chache kabla ya mechi kuisha kutokana na mashabiki wake kumvamia mwamuzi msaidizi, wachezaji na benchi la ufundi kwa mawe na chupa za maji. Kutokana na barua hiyo, sasa kundi C la michuano hiyo linabaki na timu za CS Constantinois ya Algeria inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 6, Club Africa inashika nafasi ya pili na TP Mazembe ya Kongo DR inashika nafasi ya tatu.

Dondoo za Hapa na Pale

Ruth Chepng'etich amepeperusha vyema bendera ya Kenya baada ya kunyakua taji lake la kwanza la Dubai Marathon baada ya ukame wa miaka 12 kwa kukata utepe kwa kutumia saa 2:17:07 katika mashindano yaliyofanyika mjini Dubai, huko Imarati. Wanariadha wawili wa Ethiopia Worknesh Degefa na Worknesh Edesa wamekamata nafasi ya pili na tatu kwenye mashindao hayo kwa upande wa wanawake. Katika upande wa wanaume, Getaneh Molla wa Ethiopia amechukua taji baada ya kutumia masaa 2:03:34 ambayo ni kasi ya juu zaidi ya mkimbiaji anayeshiriki marathoni kwa mara yake ya kwanza. Nafasi ya pili na ya tatu imekwenda kwa Waethiopia wengine Hepassa Negasa na Afesa Mengstu.

Wachezaji wa klabu ya Real Madrid wakinyayua Kombe

 

Kwengineko, Real Madrid imetajwa kuwa klabu tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa kampuni ya uhasibu ya Deloitte. Kabu hiyo ya Uhispania inathamani ya pauni milioni 674.6. Man U imeshuka hadi nafasi ya tatu baada ya Barcelona ambayo ni klabu nyingine kutoka Uhispania kuchukua nafasi ya pili. Kulikuwa na jumla ya vilabu sita vya ligi ya Uingereza vilivyojumuishwa katika orodha ya vilabu kumi tajiri zaidi duniani. Orodha ya klabu tajiri zaidi duniani ambayo huchapishwa kila mwaka na kampuni ya Deloitte huangazia thamani ya vilabu bila kujumuisha madeni.

Huku hayo yakirifiwa, usiku wa Januari 25 klabu ya Arsenal ilikuwa mwenyeji wa Manchester United katika uwanja wa Old Trafford kucheza mchezo wao wa Kombe la FA, ambapo Man U waliingia uwanja huo wakiwa na kocha wao wa mpito Ole Gunnar Solskjae na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kaimu Kocha Mkuu wa Man U, Ole Gunnar Solskjaer

Tangu Ole Gunnar akabidhiwe klabu ya Man U na kuiongoza kucheza mechi 8, hadi sasa amefanikiwa kushinda mechi zote huku wakifunga zaidi ya magoli 20. Katika mchezo mwingine wa Kombe la FA, klabu ya Crystal Palace iliilaza Tottenham mabao 2-0 yaliyofungwa na Connor Wickham na Andros Townsend.  Hotspurs wamebanduliwa nje ya kombe hilo kwa kichapo hicho. Siku ya Jumatano Chelsea iliifumua Sheffiel mabao 3 bila jibu.

Na klabu ya AS Monaco ya Ufaransa imempiga kalamu nyekundu kocha wao mkuu Thierry Henry, kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya. Kilichowashangaza wengi ni baada ya kumfuta kazi Henry wamemtangaza kocha wao wa zamani Leandro Jardim kuwa ndio kocha wao mpya kwa mkataba wa miaka miwili na nusu. Monaco walimfuta kazi Jardim miezi mitatu iliyopita na kumpa kazi Henry na sasa wamemfuta kazi Henry ikiwa zimepita siku 104 toka wamuajiri. Henry ambaye alikuwa na mkataba na AS Monaco hadi mwaka 2021 alijiunga na klabu hiyo mwezi Oktoba na kuanza harakati za kuipambania timu hiyo bila mafanikio na hatimae kujikuta akifungwa katika michezo 11 kati ya 20 aliyofundisha timu hiyo na kuambulia sare mechi 5 na ushindi katika michuano 4 tu.

………………….TAMATI……………