Ijumaa tarehe 8 Februari 2019
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Jamadithani 1440 Hijria sawa na Februari 8 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, wananchi na jeshi la Iran, walionyesha utiifu wao kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomein (MA). Siku hiyo mamilioni ya wananchi walipiga nara zilizoonyesha utiifu na uungaji mkono wao kwa Imamu na serikali ya Mapinduzi, kupitia maandamano makubwa yaliyofanyika katika miji tofauti ya Iran huku wakisisitiza juu ya kuendelea na mapambano hadi kuung’oa kikamilifu utawala wa Shah. Kwa upande mwingingine, maafisa na askari wa jeshi la anga wakiwa wamevalia sare za kijeshi walifika mbele ya Imam Khomein (MA) na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapinduzi ya Kiislamu. Akiwahutubia shakhsia hao, Imam alisema: “Hadi sasa mlikuwa mkimtii twaghuti, lakini kuanzia leo mmefungamana na Qur’ani. Qur’ani itawalindeni, na ninataraji kwa msaada wenu tutaweza kuweka nchini Iran utawala wa kiuadilifu wa Kiislamu.” Mwisho wa kunukuu.
Tarehe 8 Februari miaka 56 iliyopita Kanali Abdu Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa jeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa Iraq. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 781 iliyopita alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).