Jumapili, Februari 10, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 4 Mfunguo Tisa Jamaduth-Thani 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 10 Februari 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 256 iliyopita ulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa huko katika mji wa Paris. Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada. Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika kipidi hicho Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita alifariki dunia Sophia Krukovsky mwanahisabati wa Russia. Alizaliwa mwaka 1850 mjini Moscow. Licha ya kuwa alipendelea sana elimu ya hisabati, lakini kutokana na sababu za kibaguzi hakuweza kujiunga na chuo kikuu na ni kwa msingi huo ndio maana akaelekea nchini Ujerumani na kujifunza elimu ya hisabati na fizikia. Pamoja na hayo Sophia Krukovsky alikabiliwa na matatizo mengi kabla ya kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Kufuatia hali hiyo alilazimika kusoma elimu hiyo kwa mwalimu wa hisabati nje ya chuo kikuu. Mwaka 1874 Sophia Krukovsky alitunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) bila kuhudhuria chuoni. Aidha mwaka 1888 alitunukiwa zawadi yenye itibari katika chuo cha academia nchini Ufaransa. Kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1891 alipofariki dunia alijishughulisha na kazi ya ufundishaji wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa amani baina ya tawala waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia. Katika siku hii, Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza na Ufaransa zilitiliana saini mkataba na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo zilizojumuisha Italia, Finland, Poland, Bulgaria Romania na Hungary. Kwa utaratibu huo nchi hizo sita kwa mara nyingine tena zikajipatia mamlaka ya kujitawala. Hata hivyo nchi nne za Poland, Hungary, Romania na Bulgaria ambazo mwishoni mwa vita hivyo zilikuwa zimekaliwa kwa mabavu na jeshi la Umoja wa Kisovieti, zililazimika kuwa chini ya mfumo wa kikomunisti.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, yaani tarehe 10 Februari 1950 Miladia Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomunisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "McCarthyism" huko nchini Marekani, wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa nyendo zao na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomunisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya McCarthyism ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliweza kuwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita yaani tarehe 4 Jamaduth-Thani 1375 Hijiria, aliuawa shahidi pamoja na rafiki zake watatu Sayyid Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Alizaliwa katika familia ya chini hapa mjini Tehran mwaka 1303 Hijiria Shamsia na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Abadan, Iran na kisha mjini Najaf, Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, Abbas Iqbal Ashtiyani, mhakiki, mwandishi, mtambuzi wa lugha na mwanahistoria wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1275 Hijria Shamsia na baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran mwaka 1304 alifanikiwa kupata shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Sorbonne cha Ufaransa. Ashtiyani alirejea hapa nchini na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini (MA) pamoja na shakhsia wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa wanamapambano hao. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema alama za nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza njama hiyo ya majenerali wa Shah ya kutekeleza nchini sheria za kijeshi au kwa ibara yingine, sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingine.