Jumatano, 3 Aprili, 2019
Leo ni Jumatano tarehe 27 Rajab mwaka 1440 Hijria sawa na Aprili 3 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1453 iliyopita, Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad Mustafa (s.a.w) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.

Siku kama ya leo miaka 973 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf".
Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Aprili 1941, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya kujiri mapigano kati ya wazalendo wenye uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London. Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wa wake. Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili ya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa mara ya kwanza. Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran yalianza yakiwa na wafanyakazi wachache kama vile Sayyid Muhammad Ridha Shushtari, Sayyid Hashim Shushtari ambaye kwa sasa ni marehemu, Muhammad Baraza, Leyla Kimani, Said Kambi, Amir Ibrahim, Abdul Fatah Mussa na Ahmed Rashid . Watangazaji wengine wa idhaa hii ni Asmahan Ghanima Mohammad, Salum Bendera, Mubarak Henia, Sudi Ja'afar Shaban na Hussein Hassan Kamau. Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo. Kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka 1997 Radio Tehran ilianza kutangaza kwa muda wa saa moja kuanzia saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki, na matangazo hayo kurejewa siku ya pili yake kuanzia saa 12:30 asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki sawa na saa 11:30 asubuhi kwa majira ya Afrika ya Kati. Mnamo tarehe 23 Mfunguo Tatu (Dhulhijja) 1418 Hijria iliyosadifiana na tarehe 21 Aprili 1998 Milaadia, matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa hewani kwa muda wa masaa matatu katika nyakati za usiku, asubuhi na machana. Saa moja ilikuwa ni marudio ya matangazo ya asubuhi, ambayo yalikuwa yakisikika kuanzia saa saba kamili hadi saa nane kamili mchana kila siku kwa majira ya Afrika Mashariki. Kwa hivi sasa Idhaa imeongeza wafanyakazi wake ambapo matangazo ya mchana nayo sasa yanasikika kwa njia ya moja kwa moja kuanzia saa 5:30 hadi 6:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki. Inarusha matangazo yake kwa ajili ya nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, mashariki mwa Zambia, kaskazini mwa Malawi na Msumbiji pamoja na Afrika Kusini. Inarusha pia matangazo yake kwa ajili ya nchi za Mashariki ya Kati hususan za Ghuba ya Uajemi na ina waandishi wake katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati kama vile Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Kongo. Matangazo ya IRIB yanalenga kusambaza habari juu ya Iran na utamaduni wake. Yanalenga kusambaza mitazamo ya Kiislamu na mafundisho ya Ahlul Baiti (as) inayolingana na siasa ya Iran. Matangazo ya IRIB pia yananawabaishia Walimwengu ubeberu wa Marekani na madola ya Kimagharibi dhidi ya mataifa mengine na ukandamizaji wa utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina. ***
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, inayosadifiana na 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuizuia Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.
