Ijumaa, Aprili 5, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 29 ya mwezi Rajab 1440 Hijria ambayo inalingana na tarehe 5 Aprili 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1164 iliyopita sawa na tarehe 29 Rajab mwaka 276 Hijria, aliaga dunia Abdullah bin Muslim Dinuri, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63. Ibn Qutayba alizaliwa mjini Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinuri, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi. Alimu huyo aliandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Ghariibul-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.” ***
Katika siku kama ya leo miaka 561 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Shamsuddeen, fakihi na mfasiri wa kiislamu. Msomi huyo aliaga dunia huko Halab moja ya miji ya Syria. Shamsuddeen alisoma fikihi na tafsiri ya Qur'ani kwa Ibn Hammam, fakihi na msomi mahiri wa zama hizo. Msomi huyo baadaye alijishughulisha na taaluma ya uandishi vitabu na kuandika vitabu vyenye thamani katika uga wa mafundisho ya Kiislamu. Al-Taqrir wat-Ta'abir ni moja ya vitabu muuhi9mu vya mwanazuoni huyo. ***
Siku kama ya leo miaka 434 inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Haarlem nchini Uholanzi, ambako kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Uhispania 1609. ***
Miaka 225 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Georges Danton, aliyekuwa miongoni mwa vinara wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mahiri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kumtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa. ***
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, aliaga dunia Muhammad Ali Shah, mfalme dhalimu wa ukoo wa Qajar nchini Iran. Muhammad Ali Shah alizaliwa 1249 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz na baada ya kusoma kidogo, akiwa na umri wa miaka 17 alianza kufanya kazi yake ya kwanza serikalini. Baada ya Mozaffar ad-Din Shah Qajar kuingia madarakani, Muhammad Ali Shah aliteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. ***
Na siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi ya utawala ghasibu wa Israel, siku ya tarehe 4 Aprili, yaliwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni. ***