Apr 29, 2019 04:16 UTC
  • Jumapili, tarehe 28, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 22 Sha'ban 1440 Hijiria, sawa na tarehe 28 Aprili 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 852 iliyopita alifariki dunia Ibn Shahr Ashub, alimu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya hadithi. Muhammad Bin Ali Ibn Shahr Ashub alizaliwa katika mji wa Mazandaran nchini Iran na kupewa jina la Ibn Shahr Ashub kama ambavyo pia alipewa lakabu ya 'Zainud-Din na Rashidud-Din,' ambapo alitambuliwa kuwa na upeo wa juu wa elimu ya theolojia, hatibu, mtaalamu wa elimu ya fasihi na kadhi mashuhuri wa Waislamu wa Kishia. Kutokana na masuala ya kimadh'hab, Ibn Shahr Ashub alilazimika kuondoka Iran  katika kipindi cha utawala wa Maseljuq na kukimbilia mjini Aleppo, Syria ya leo. Aliheshimiwa sana na hata wasomi wakubwa wa Kisuni wa zama zake. Ibn Shahr Ashub alipewa idhini ya kupokeza hadithi na maulama wakubwa wa zama zake kama vile Zamakhshari, Imam Muhammad Ghazali na Khatwib Khawarazmi. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Maalimul-Ulamaa' 'Manaaqib Aali Abi Twalib' 'Mutashaabihul-Qur'an' na 'Al-Arbaiin.'

Ibn Shahr Ashub

Siku kama ya leo miaka 667 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba alifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.

Ibn Hajar Asqalani

Siku kama ya leo miaka 464 iliyopita, Kongamano la Augsburg lilifanyika katika mji wenye jina hilo huko nchini Ujerumani. Katika kongamano hilo, viongozi wa Kikatoliki chini ya uongozi wa Papa Paul IV (wa Nne) kwa mara ya kwanza waliunga mkono uhuru wa madhehebu ya Waprotestanti. Katika kongamano hilo pia ulichukuliwa uamuzi wa kurejeshwa mali za Waprotestanti walizokuwa wamenyang'anywa. Hata hivyo uamuzi huo haukutekelezwa na hivyo kuzusha vita vya miaka kumi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika nchi mbalimbali za Ulaya.

Kongamano la Augsburg

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita alifariki dunia Allamah Sheikh Muhammad Jawad Balaghi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Katika zama zake alikuwa mtaalamu wa elimu ya fiqhi, mwalimu na mwandishi mkubwa. Allamah Balaghi alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Mirza Shirazi na kutokea kuwa mmoja wa walimu na waandishi wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Balaghul-Mubin' kinachothibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Allamah Sheikh Muhammad Jawad Balaghi,

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, Benito Mussolini dikteta wa Kifashisti wa Italia aliuawa kwa kunyongwa na wazalendo wa nchi hiyo. Mussolini alizaliwa Julai 29 mwaka 1883 katika familia masikini huko kaskazini mwa Italia. Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu alianza kufanya kazi ya uandishi katika magazeti. Machi 23 mwaka 1919 Mussolini alistafidi na uasi na hali ya vurugu iliyojitokeza  nchini italia na kuanzisha Chama cha Ufashisti na kuwa kiongozi wa chama hicho. Ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa 1922 ulimfanya Benito Mussolini kuwa Waziri Mkuu baada ya kumridhisha mfalme.

Dikteta Benito Mussolini

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha. Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomonisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia. Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani akawaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam.

Vita vya Marekani nchini Vietnam

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, yaani tarehe 8 Ordibehesht, watawala wa kizazi cha Aal Saud walikata uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya utawala wa Saudia kufanya mauaji ya umati ya mahujaji wa Wairani wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka katika siku iliyopewa jina la Ijumaa ya Damu hapo tarehe 9 Mordad 1366 Hijria Shamsia, uhusiano wa Iran na nchi hiyo ulifika kiwango cha chini zaidi na wanadiplomasia wa Iran nchini Saudia wakapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Wanadiplomasia wa Saudia mjini Tehran walikuwa tayari wamekwishaondoka. Hatimaye uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa kikamilifu tarehe 28 Aprili 1986. Safari za Wairani waliokuwa na hamu ya kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka na Haram tukufu ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina pia zilisimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa katika kipindi ambacho Saudi Arabia ilikuwa msaidizi mkubwa wa kifedha wa utawla wa Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran na hatua hiyo ilichukuliwa sambamba na siasa za Marekani za kubana na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mauaji ya umati ya watawala wa Aal-Saud dhidi ya mahujaji wa Iran

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali kibaraka ya nchi hiyo. Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani. Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan.

Bendera ya Afghanistan