Jun 25, 2019 13:58 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 22 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Tulisema katika kipindi kilichopita kuwa wanawake wa Iran walikuwa na nafasi chanya, athirifu na muhimu zaidi katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo Imam Khomeini (MA) alikuwa akisisitiza mara kwa mara nafasi hiyo, huku akiitaja sehemu tofauti katika kipindi cha Mwamko wa Mapinduzi kuwa iliyozidi nafasi ya wanaume. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, ni wanawake hao ndio kwa kujitolea na ushujaa wao walikuwa wakiwashajiisha wanaume na kupelekea kupatikana umoja na mshikamano katika safu za wanamapinduzi. Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa chachu ya kupatikana uhuru na uadilifu wa kijamii, sanjari na kupatikana mfumo ambao uliandaa mazingira ya kufikiwa haki za kisiasa na kijamii za wanawake, kama ambavyo  pia yalihuisha izza na utukufu wao. Nafasi chanya ya wanawake nchini Iran haikukomea katika matukio ya mwamko wa Mapinduzi pekee, bali hadi mwisho wa uhai wa utawala wa kidikteta, nafasi hiyo muhimu ya wanawake ilihisika katika nyanja zake tofauti kisiasa na hata kijamii nchini hapa. Kwa kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, kupitia uhuru, kujiamini na heshima yao iliyofikiwa kutokana na ushindi wa Mapinduzi, wanawake waliweza kuwa na nafasi na madaraka katika sekta tofauti.

Wanawake wa Iran wapo katika kila sekta na hawajarudi nyuma katu

Katika uwanja huo, Imam Khomeini anasema: “Hii leo na kwa baraka za Mwamko wa Kiislamu, mwanamke ni mwakilishi athirifu wa jamii kwa kuweza kutumia vyema nafasia yake. Wanawake ni mashujaa na walishirikiana bega kwa bega na wanaume katika ujenzi wa Iran na kadhalika katika kujijenga wao wenyewe katika elimu na utamaduni. Na hakuna miji au vijiji vinavyoonekana ila kuna makundi na jumuiya muhimu za wanawake ambao wanajishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kielimu yamefikiwa kwa juhudi za wanawake waaminifu wa Kiislamu. Kwa hakika Mwamko wa Kiislamu uliopatikana kwa baraka za Uislamu, ndio umeleta mabadiliko haya ndani ya nafsi za wanawake na wanaume katika jamii….Hii leo wanawake ndani ya Jamhuri ya Kiislamu wanafanya juhudi mbalimbali pamoja na wanaume kwa ajili ya kujijenga wao wenyewe na nchi yao, na hii ina maana ya kupatikana ‘uhuru halisi wa wanawake’ na ‘uhuru halisi wa wanaume’ sio kile kilichokuwa kikisemwa katika kipindi cha utawala wa Shah cha uhuru chini ya kifungo, mateso na adhabu.” Ujumbe wa imam kwa mnasaba wa siku ya mwanamke wa tarehe 15/2/1359.

*****

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 22 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia matukio na nafasi muhimu za shakhsia tofauti katika kipindi cha kujiri Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Moja ya mafanikio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu, ni kupatikana uhuru halisi kwa manufaa ya wanawake. Akijibu swali la wale ambao katika kipindi cha Mwamko wa Kiislamu walihoji juu ya nafasi na hadhi ya mwanamke katika utawala wa Kiislamu, Imam Khomeini daima alikuwa akisema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ingeandaa nyanja tofauti za kuwepo na kushiriki wanawake katika nyuga tofauti serikalini. Aidha akijibu swali la waandishi wawili wa habari wa gazeti kongwe la al-Ahram na mwingine kutoka Japan kuhusiana na suala hilo alisema: “Uislamu si tu kwamba unakubaliana na uhuru wa mwanamke, bali wenyewe ndio mwasisi wa uhuru wa mwanamke katika nyanja zote zinazomuhusu mwanamke.

Mwanamke wa Iran yupo huru katika kila sekta maadamu tu ni katika masuala yasiyomuudhi Muumba

Wanawake wako huru kushiriki katika masuala mengi. Uhuru kwa maana yake halisi na sio kama ule uliokuwa ukidaiwa na Shah.” Mahojiano ya tarehe 25/10/1357. Kadhalika akijibu swali la mwandishi mwingine wa habari ambaye naye alitaka kujua nafasi ya wanawake katika serikali ya Jamhuri ya Kiislamu, Imam alisema kuwa kuchunga heshima na kujistiri katika jamii ni mambo ya lazima yanayoandamana na uhuru wa wanawake na kuhusu hilo alisema: “Nafasi ya wanawake katika serikali, ina maana ya kumfanya kuwa mwanadamu sahihi na shakhsia huru, kinyume na vipindi vilivyopita ambapo wanawake wetu hawakuwa huru wala wanaume wetu. Na kuanzia sasa wanawake wako huru lakini iwapo watataka kufanya kazi zao kinyume na ifa na kujistiri au kinyume na maslahi, basi watazuiliwa.” Mahojiano na waandishi wa habari baada ya Shah kukimbia nchi ya tarehe 27/10/1357.

******

Moja ya nyanja muhimu na za kuvutia za nafasi ya wanawake katika nyuga tofauti za kijamii katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni ushiriki wao katika ‘Jihadi ya Ujenzi.’ Jihadi ya ujenzi wa taifa iliundwa kwa amri ya Imam Khomeini kwa lengo la kutokomeza umasikini na hali ngumu katika maeneo tofauti ya watu wasiojiweza nchini, ambapo tangu mwanzoni mwa kuasisiwa mfumo mpya wa Kiislamu nchini iliwahusisha watu wote na kwa ari ya juu. Baada ya kutolewa amri ya kuundwa Jihadi ya Ujenzi wa Taifa, wanawake kwa kushirikiana na wanaume na kwa lengo la kufikiwa uadilifu wa kijamii walifanya juhudi kubwa ya kutokomeza umasikini na hali ngumu katika maeneo ya watu masikini. Huku akipongeza ari na mwamko wa hali ya juu wa wanawake katika ushiriki wao ndani ya taasisi hiyo muhimu ya ujenzi wa taifa Imam (MA) alisema kuwa hatua yao hiyo ilikuwa nzuri na yenye thamani kubwa na kuongeza kusema: “Bila shaka hii ilikuwa irada ya Mwenyezi Mungu, ilikuwa nguvu isiyo ya kawaida. Hakuna nguvu nyingine inayoweza kufanikisha jambo hili, kiasi cha kuwavutia vijana na wanawake kushiriki katika jihadi ya ujenzi wa taifa. Wanawake ambao wakati huo hawakuwa wakijali, bila kubaki nyuma waliingia katika ujenzi wa nchi na masuala yote muhimu, na tuliona pia jinzi wanavyoweza kutekeleza vyema majukumu yao. Wakati wakulima wanapoona idadi kubwa ya wanawake wakitoka nje ya nyumba zao na kwenda kusaidia (kilimo) kitendo hicho huwa  na taathira kubwa kwa wakulima hao na kwa hakika huwa na thamani kubwa.” Hotuba ya Imam Khomeini ya tarehe 27/6/1358.

Wanawake wa Iran wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha Ushindi wa Mapinduzi ya Iran

Wanawake mbali na kuwa na nafasi chanya katika taasisi ya Jihadi ya Ujenzi wa Taifa, pia walihusika kwa kiasi kikubwa katika ulinzi wa nchi katika kipindi cha vita vya kulazimishwa. Akizungumzia nafasi ya wanawake katika kuwasaidia wapiganaji katika kipindi cha kujitetea kutakatifu Imam anasema: “Katika kipindi fulani ambapo tulikuwa katika matatizo yaliyozushwa na madola maovu, huku Iran ikishambuliwa kila upande, nyinyi wanawake mlikuwa nyuma ya ulingo wa vita mkijishughulisha, mwamko huo ulikuwa wa ulingo wa vita ….” Hotuba ya tarehe 7/8/1359.

*****

Aidha Imam Khomeini (MA) alizungumzia nafasi athirifu ya uungaji mkono wa wanawake katika kuwasaidia wapiganaji katika vita vya kulazimishwa kuwa isiyo na mfano wake katika historia kwa kusema: “Wakati ninapoona kwenye televishani kundi la wanawake limekaa katika moja ya miji likiwaokea mikate vijana ambao walikuwa wakipambana katika medani ya vita kwa ukamilifu huku mikononi mwao wakiwa wamebeba mifuko (ya mikate) ninahisi aibu na kujiuliza sisi (wanaume) tuko wapi (daraja ya kujitolea) na hawa wanawake wako wapi? Tizameni katika historia tangu mwanzoni mwa historia hadi leo, mmewahi kushuhudia wanawake hususan wanawake vijana, badala ya wao kwenda kujishughulisha na ujana wao, wanafanya juhudi kubwa kiasi hiki katika kulisaidia jeshi? Je, nyinyi (wanaume) mko wapi?” Hotuba ya Imam ya tarehe 7/8/1359.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 22 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.