Jun 25, 2019 14:19 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 24 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, serikali ya Kiislam inalo jukumu la kuandaa mazingira bora yatakayowafanya wanawake waweze kufikia nafasi muhimu zaheshima na kibinaadamu katika jamii. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo, hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi.

Ndugu wasikilizaji, akijibu swali la George Guerre mwandishi wa habari wa gazeti la The Los Angeles Times la nchini Marekani ambaye alihoji kuhusiana na mustakbali wa ushiriki wa wanawake katika vyuo vikuu na kushiriki darasa moja na wanaume na kadhlika suala la udhibiti wa uzazi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) alisema: “Wanawake katika jamii ya Kiislamu wako huru na ushiriki wao katika vyuo vikuu, ofisini na bungeni hauzuiliwi kwa njia yoyote ile. Kile kinachozuiliwa ni ufisadi wa kiakhlaqi ambao ni haramu kwa mwanaume na mwanamke. Ama kuhusu uzazi, utazingatia kile ambacho kinaainishwa na serikali.” 

Wanawake wa Iran mashujaa

Hotuba ya tarehe 16/6/1357. Imam Khomeini sambamba na kutetea haki za wanawake, bila kuogopa mashinikizo ya kisaikolojia na kipropaganda ya serikali tofauti za kigeni, alitangaza wazi upinzani wake kuhusiana na baadhi ya masuala ambayo yametangazwa katika nchi za Magharibi kuwa eti ni haki za wanawake na kusema kuwa masuala hayo hayakubaliki katika mtazamo wa Uislamu.

******

Kwa mfano, katika mahojiano hayo Imam Khomeini hakuunga mkono suala la kuavya mimba kuwa ni haki ya wanawake na badala yake alikitaja kitendo hicho kuwa ni haramu kwa mtazamo wa Uislamu sambamba na kubainisha sheria zake. Akijibu swali la mwandishi wa habari wa gazeti la Uholanzi la Holland Dewel Grant ambaye alimtaka Imam afafanue haki za wanawake katika Jamhuri ya Kiislamu na pia suala la kuavya mimba, alisema: “Kwa mtazamo wa haki za binaadamu, hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanamume kwa kuwa wote wawili ni wanadamu na katika hilo mwanamke anayo haki ya kuingilia mustakbali wake kama ilivyo kwa mwanamume. Hata hivyo katika baadhi ya mambo kuna utofauti kati ya mwanamume na mwanamke ambayo haihusiani na utambulisho wao. Kwani masuala ya utambulisho na utukufu hayapingani na utu mwanamke. Ama kuhusu kuavya mimba, mtazamo wa Kiislamu ni kwamba suala hilo ni haramu.” Mahojiano ya tarehe 16/8/1357.

Wanawake wa Iran wakiwa wenye furaha kutokana na kutonyanyaswa na serikali ya Kiislamu

Kadhalika Imam akiwajibu watu ambao walionyesha kuwa na wasi wasi kutokana na kusimamishwa mfumo wa Kiislamu nchini Iran na kulitaja suala la kuvaa hijabu na baibui kwa wanawake kuwa la lazima, alitetea mavazi hayo ya wanawake ingawa hakusema kuwa ni lazima liwe tu vazi la baibui. Aidha katika mahojiano na DR Jim Kukle, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Rutgers cha nchini Marekani kuhusiana na pande tofauti za haki za kijamii za wanawake hususan suala la kuwalazimisha kuvaa baibui sambamba na kukosoa kile alichokiita kuwa eti ni kumgeuza mwanamke kuwa sawa na kitu kisicho na thamani katika jamii, Imam Khomeini alisisitiza kuwa wadhifa wa serikali ya Kiislamu ni kumtetea mwanamke kwa ajili ya kumbadili kuwa mwanadamu halisi mwenye thamani kwa kusema: “Mwanamke ni kama mwanaume katika masuala kama vile kusoma katika chuo kikuu, kufanya kazi za serikali na kusafiri, yupo huru. Kamwe mwanamke hana tofauti na mwanamume. Ndio! Katika Uislamu ni lazima mwanamke awe na hijabu lakini sio lazima hijabu hiyo iwe ni baibui, bali mwanamke anaweza kujisitiri kwa vazi lolote lile. Sisi hatuwezi na pia Uislamu hautaki kumfanya mwanamke kuwa kitu chochote au kumfanya kuwa doli. Uislamu unataka kulinda shakhsia ya mwanamke na kumjenga kuwa mwanadamu halisi mwenye hadhi. Sisi kamwe hatutoruhusu mwanamke kuwa chombo tu kinachotumiwa na wanaume kwa ajili ya kukidhia haja zao za kimatamanio. Aidha Uislamu unakuchukulia kuavya mimba kuwa ni haramu." Mahojiano ya tarehe 7/10/1357.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilichoko hewani ni sehemu ya 24 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia nadharia na mitazamo ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Ndugu wasikilizaji haki ya talaka kwa ajili ya wanawake ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo yaliulizwa sana na hata kuibua mjadala mkubwa kati ya waandishi wa habari na Imam Khomeini (MA). Itakumbukwa kuwa katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi hususan za Magharibi, zimewapa wanawake haki ya kudai talaka sambamba na kutolewa madai kwamba, dini ya Kiislamu imewanyima kabisa wanawake haki hiyo. Katika uwanja huo Wamagharibi wanahoji kwamba, hatua ya Uislamu kukabidhi mamlaka ya talaka kwa wanaume pekee, imepelekea kukanyagwa haki ya wanawake. Imam Khomeini (MA)  alitumia mantiki kujibu hoja hiyo ambapo sambamba na kutetea haki ya talaka kupewa wanaume aliashiria suala hilo kupitia haki na sheria ya ndoa katika mfumo wa Kiislamu kwa madhumuni ya kuwafanya wanawake wanufaike  na haki hiyo.

Wanawake wa Iran ambao hawajaachwa nyuma hata chembe

Kwa mfano,  akizungumza na wanawake wa mji wa Qum Imam Khomeini alisema: “Wanawake wanaotaka kuolewa tangu mwanzo wanaweza kujipa hiari ambazo hazipingani na sheria wala heshima zao. Kwa mfano wanaweza kushurutisha tangu mwanzo kwamba iwapo maume zao watakuwa na tabia mbaya au kuwafanyia miamala mibaya wake zao, basi wake hao watakuwa mawakili wa nafsi zao katika kufuatilia talaka. Uislamu umempa mwanamke haki ya kujiamulia kuhusu suala hilo. Inapoonekana kuwa Uislamu umewawekea mipaka wanawake na wanaume, basi ifahamike kuwa mipaka hiyo ni kwa maslahi yao wenyewe.” Hotuba ya tarehe 15/12/1357. Aidha katika kikao hicho hicho Imam alibainisha kipengee cha sharti la uwakili katika ndoa kwa ajili ya kumsaidia mwanamke kufikia haki yake ya kupata talaka kupitia mujtahidi na walii mtaalamu wa sheria kwa kusema tena: “Kwa kutilia maanani kwamba haki ya uwakili wa talaka katika ndoa imepewa mwanamke, mwanaume hawezi tena kumtenga (kumdhulumu) mwanamke huyo. Iwapo mume atamfanyia tabia mbaya (kuudhi/kutesa) mwanamke, katika Uislamu mwanamume huyo huonywa. Na iwapo hasikii basi anawekewa hadi (anaadhibiwa) na ikiwa pia hakusikia, basi mujtahidi hutoa talaka kwa mwanamke (hata kama mume hakuridhika).” Hotuba ya tarehe 15/12/1357.

*******

Kadhalika akijibu suala kwamba kubakia haki ya talaka mikononi mwa wanaume limeudhi na kuleta suitafahamu kwa kundi fulani la wanawake wanamapambano nchini Iran, na kwamba kuna watu wanaotumia vibaya suala hilo kuwachochea wanawake wadhanie kuwa hawatoweza tena kuwa na uwezo wa kujichukulia talaka, Imam Khomeini alisema: “Wanawake watukufu wamewekewa njia nyepesi na maalumu ambayo wataweza kujichukulia talaka. Hii ikiwa na maana kwamba ikiwa katika ndoa kutawekwa sharti la mwanamke kujipa uwakili wa talaka kwa sababu yoyote ile, yaani wakati wowote ule atakaotaka kuchukua talaka au kwa masharti maalum, kwa mfano ikiwa mumewe atamfanyia tabia mbaya (kumuudhi), kumuoa mke mwingine na kadhalika, basi mwanamke atakuwa na hiari ya uwakili wa talaka na katika hilo hakutakuwa na tatizo lolote kwa wanawake kujipa talaka.”

Wanawake wa Iran katika uga wa kimaanawi

Ama suala lingine muhimu kuhusu haki za mwanamke katika serikali ya Kiislamu ni kadhia ya kugharamia mahitaji ya mwanamke. Kwa msingi wa mafundisho ya Uislamu, ni jukumu la mwanaume kuwadhaminia mke na watoto wake mahitaji ya maisha yao. Hata wakati ambapo mwanamke atakuwa na kipato cha kutosha, bado mahitaji yake yanatatakiwa kukidhiwa na mumewe. Akijibu swali kwamba je, iwapo mwanamke atakuwa anajitosheleza kwa kipato chake, bado mumewe atahitajika kumdhaminia mahitaji yake, Imam Khomeini (MA) alijibu kwa kusema: “Ni wajibu kwa mume kumkidhia mkewe mahitaji yake ya maisha, hata kama mke huyo atakuwa na kipato cha kutosha.”

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 24 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

 

 

Tags