Jun 27, 2019 05:59 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 831 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 49 hadi 51 ambazo zinasema:

هَذَا ذِكْرٌ وَإِنَّ لِلْمُتَّقِينَ لَحُسْنَ مَآبٍ

Huu ni ukumbusho. Na hakika wachamngu wana marudio mazuri.

جَنَّاتِ عَدْنٍ مُّفَتَّحَةً لَّهُمُ الأَبْوَابُ

Bustani za milele zitazo funguliwa milango yao kwa ajili yao.

مُتَّكِئِينَ فِيهَا يَدْعُونَ فِيهَا بِفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ وَشَرَابٍ

Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulisoma aya zilizozungumzia habari za baadhi ya Mitume wa Allah. Aya hizi tulizosoma, kwanza zinafanya hitimisho la aya zilizotangulia kwa kusema: Lengo la kuzungumziwa habari za waliopita ni kuaidhi na kutoa nasaha kwa kukumbusha, kwa sababu moja ya madhumuni ya kuteremshwa Qur'ani ni kuaidhi na kukumbusha. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu si kwa ajili ya Mitume peke yao, bali hata watu wengine wanaoshikamana na taqwa na wakamcha Mungu, watakuwa na mwisho mwema pia. Allah SW atawafidia Siku ya Kiyama kwa tabu mbali mbali walizopata duniani na atawapa malipo ya thawabu kwa mema waliyofanya. Ikiwa hapa duniani walijihini na kusamehe baadhi ya raha na starehe kwa sababu ya kuchunga halali na haramu, Siku ya Kiyama, Allah atawaneemesha kwa neema bora na kubwa kabisa za raha na starehe. Isitoshe, raha na starehe za dunia ni za kupita, na zinakwisha kwa mtu kupatwa na maradhi na mauti, lakini Pepo na raha zake ni za milele, wala hazina mwisho wala kumalizika. Wale ambao hapa duniani walikuwa muda wote wakijipinda kufanya mema na kujiepusha na mabaya, Siku ya Kiyama, Allah SW atawaandalia makazi mema ili uweze kuthibiti uadilifu wake Mola kwa waja wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kusimuliwa historia ya waliotangulia hakufanywi kwa madhumuni ya kuburudisha, bali inapasa simulizi hizo zimzindue na kumwamsha mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, umri mrefu si jambo muhimu sana, la msingi na muhimu zaidi ni hatima na mwisho wa maisha ya mtu. Taqwa na ucha Mungu ndio wenzo wa kuwa na mwisho mwema. Kwa hivyo wenye taqwa na wamchao Mwenyezi Mungu ndio watu pekee ambao Mola ameahidi kwamba, watakuwa na mwisho mwema. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, milango ya rehma za Allah iko wazi kwa watu wa Peponi; na chochote watakachotaka watakipata na kuneemeka nacho huko Peponi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 52 hadi 54 ambazo zinasema:

وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ أَتْرَابٌ

Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu zao.

هَذَا مَا تُوعَدُونَ لِيَوْمِ الْحِسَابِ

Haya ndiyo mliyo ahidiwa kwa Siku ya Hisabu.

إِنَّ هَذَا لَرِزْقُنَا مَا لَهُ مِن نَّفَادٍ

Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu neema za Peponi kwa kuashiria hitajio la kuwa na mke atakalokuwa nalo mtu hata huko Peponi na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu amewawekea watu wa Peponi wake wazuri na jamili, wasafi na waliotakasika, ambao hawashughulishwi na yeyote yule isipokuwa waume zao, na watakuwa na umri sawa na wao. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, katika siku hiyo ya hesabu ambayo iko kwa ajili ya watu wote, ambapo watu watapaswa kuwajibika kwa amali na matendo waliyofanya duniani, ni wale waliomcha Mwenyezi Mungu tu ndio watakaoneemeka kwa neema za Peponi. Ahadi ya Allah kuhusiana na watu hao itathibiti, kwani Yeye Mola katu hayakhalifu wala haendi kinyume na yale aliyoyaahidi. Nukta nyingine ni kwamba, neema na riziki watakazotunukiwa watu wa Peponi hazina mwisho wala hazimaliziki. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, sifa ya mke mzuri na mwema ni kutovutiwa na yeyote mwengine ghairi ya mume wake na moyo wake kutotekwa na mwingine yeyote asiyekuwa yeye. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, neema za Peponi ni za kudumu na zinatolewa kwa mazingatio ya amali za watu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, maadi, yaani kufufuliwa viumbe kutakuwa kwa sura ya kimwili pia, si kiroho pekee. Yaani watu watakuwa na viwiliwili vinavyoshabihiana na vile walivyokuwa navyo duniani. Huko wataburudika kwa kula matunda yenye ladha tamu ya ajabu na kunywa vinywaji vya kuburudisha mno. Aidha wataweza kukidhi matamanio yao ya kijinsia kwa kutunukiwa wake wenye jamali na uzuri usio na kifani.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 55 hadi 58 za sura yetu ya S'aad ambazo zinasema:

هَذَا وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ

Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa;

جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ

Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nayo ni malalo maovu mno.

هَذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌ وَغَسَّاقٌ

Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!

وَآخَرُ مِن شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ​​​​​​​

Na adhabu nyenginezo za namna hii.

Utaratibu unaotumiwa na Qur'ani ni kufuatanisha habari za mwisho wa watu wema na wabaya, ili wale inaowahutubu walinganishe hali mbili hizo, kisha wachague kwa uelewa kamili njia ya maisha wanayoamua kufuata. Katika aya tulizosoma pia, baada ya kuzungumziwa neema mbali mbali watakazoneemeka nazo watu wa Peponi, Qur'ani tukufu inasema: Lakini wale waliochupa mipaka, wakaasi na kukhalifu amri za Mola wao, watapata adhabu kali Siku ya Kiyama. Badala ya vinywaji vitamu na vya kuburudisha vya Peponi, watakunywa maji yanayochemka pamoja na usaha unaochuruzika kutoka kwenye viwiliwili vyao. Makazi ya watu hao ni motoni, mahali watakakokusanywa wabaya wote, ambako kutakuwa kunanuka harufu chafu na ya uvundo wa viwiliwili vyao. Bila ya shaka adhabu ya watu wa motoni haitakuwa ya kinywaji cha maji yanayochemka na moto unaounguza tu, lakini kutakuwa na aina na namna nyingine chungu nzima za adhabu, ambazo zitawafanya watu hao wawe kwenye hilaki na mateso muda wote, na wala haitatokea katu kwa wao kuzizoea adhabu hizo na kuwa jambo la kawaida kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutafakari juu ya mwisho na hatima, humfanya mtu awe makini katika kuchagua njia ya maisha na kujiepusha na kuasi na kukhalifu kutekeleza maamrisho ya Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu za Mwenyezi Mungu ni za aina na namna mbali mbali, kama yalivyo malipo mema ya thawabu; na adhabu hizo katu hazitazoeleka wala kuvumilika kwa watu wa motoni. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujihadhari kwa kutohitari na kufadhilisha adhabu kali na ya milele ya Kiyama, kwa sababu ya raha za muda na starehe za kupita za dunia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 831 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, ayapokee mema yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/    

 

Tags