Aug 12, 2019 02:41 UTC
  • Jumatatu,  12 Agosti, mwaka 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Dhulhija mwaka 1440 Hijria sawa na Agosti 12 mwaka 2019.

Leo tarehe 10 Dhilhaj ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka, huchinja mnyama kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mola wao na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii Mtukufu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu aliijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mwanawe kipenzi Ismail (as). Licha ya mashaka ya utekelezwaji wa amri hiyo, Nabii Ibrahimu (as) aliandaa mazingira ya kutekeleza amri hiyo na kumlaza chini mwanaye na kuanza kuikata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja. Hapo ndipo alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amefaulu mtihani huo na akamtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawapa wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Tarehe 10 Dhulhija miaka 4 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na azembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia. Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.

Maafa ya Mina

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa. Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao, vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia. Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili. Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikabili tabaka hilo muhimu.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati. Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.

Mauaji ya Wapalestina katika kambi ya wakimbizi ya Tel al Zaatar

Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 yaani miaka 70 iliyopita, hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Hati hiyo ilibuniwa kufuatia mienendo isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zenye mateka zilitakiwa kuwasilisha orodha ya majina ya mateka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani. Hata hivyo licha kuweko makubaliano hayo, lakini madola mengi duniani yamekuwa yakipuuza na kukanyaga haki za mateka na majeruhi wa kivita.

 

Tags