Sep 02, 2019 04:05 UTC
  • Jumatatu tarehe Pili Septemba 2019

Leo ni Jumatatu tarehe Pili, Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba Pili mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuzingirwa katika jangwa na Karbala.

Siku kama ya leo miaka 218 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu nchini Misri. Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yakiwa hatarini. Ni kwa sababgu hiyo, ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisisonge mbele. 

Bendera ya Misri

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1805 na kuonyesha kuwa mwerevu na mwenye kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa mjiaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu.

William Rowan Hamilton

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani sawa na tarehe Pili Septemba 1945 nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19. Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Katika kipindi hicho harakati ya mapambano ya India na China kwa kuongozwa na Ho Chi Minh, ilifanikiwa kuidhibiti Vietnam na katika siku kama ya leo kukatangazwa kuasisiwa jamhuri ya Vietnam, huku miezi michache baadaye Ho Chi Minh akitangazwa kuwa rais wa nchi hiyo.

Bendera ya Vietnam 

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote. Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya Waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki. Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi Waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani Douglas MacArthur akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan. Mwaka 1951, nchi 49 duniani, zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Japan ilisalimu amri katika Vita vya Pili vya Dunia

Na tarehe 19 Shahivar miaka 57 iliyopita mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 7.3 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika eneo la Buin Zahra huko kaskazini magharibi mwa Iran. Mtetemeko huo mkubwa uliua zaidi ya watu elfu 20 na kujeruhi maelfu ya wengine. Mtetemeko huo wa ardhi ulitokea nyakati za usiku na hivyo haukuwapa watu fursa ua kuokoa maisha yao.

Mtetemeko huo wa Buin Zahra uliharibu kabisa vijiji 120 na kusababisha hasara kubwa katika mamia ya nyumba za eneo hilo. Baada tu ya mtetemeko huo wananchi wa Iran waliharakia kuwapelekea misaada wenzao wa Buin Zahra.

Mtetemeko wa ardhi wa Buin Zahra, kaskazini mwa Iran

 

Tags