Sep 21, 2019 04:30 UTC
  • Jumamosi, 21 Septemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 21 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria mwafaka na tarehe 21 Septemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 715 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli. Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Aliandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qurani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntahaal Matwalib'.***

Allamah Hilli

Katika siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha. ***

Sir Walter Scott

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Dakta Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkurumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU. ***

Kwame Nkrumah

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine. ***

Marufuku ya kuvaa hijabu katika shule za Ufaransa.

 

Tags