Jumatatu, Septemba 30, 2019
Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria sawa na Septemba 30 mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya kiongozi huyo wa Waislamu. Katika kipindi cha utawala wa Khalifa Othman bin Affan, Muawiya alikuwa gavana wa Sham na baada ya kifo cha Othman alikusudia kuwa na udhibiti katika maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu na kisha airithishe familia yake utawala huo. Vita vya Muawiya dhidi ya Imam Ali as pia vilitokana na jambo hilo.
Tarehe Mosi Safar miaka 1380 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid, suala ambalolilizusha hasira kubwa dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita kulifanyika mkutano wa kihistoria wa Munich huko Ujerumani. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja viongozi wa Ujerumani Adolph Hitler, kiongozi wa Italia Benito Mussolini na mawaziri wakuu wa wakati huo wa Uingereza na Ufaransa. Lengo la mkutano huo lilikuwa kutafuta njia ya kutatua hitilafu za Ujerumani na Czechoslovakia. Matokeo ya mkutano huo yalikuwa kumegwa sehemu ya ardhi ya Czechoslovakia na kuunganishwa na Ujerumani. Mkataba huo ulikuwa na taathira kubwa katika matukio ya baadaye barani Ulaya na ulidhihirisha zaidi sura na tabia ya kikoloni ya nchi za Magharibi. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Ujerumani hapo mwaka 1945, Czechoslovakia ilichukua tena sehemu hiyo ya ardhi.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita nchi ya Botswana ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Mwaka 1885 Botswana iliwekwa katika himaya ya Uingereza. Mapambano ya wapigania uhuru nchini humo yalishadidi tangu mwaka 1920 na mwaka 1966 nchi hiyo ilipata uhuru. Botswana inapatikana kusini mwa bara la Afrika na inapakana na nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mitetemeko ya ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mitetemeko hiyo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa mujibu wa athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.
Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina la Siku ya Kimataifa ya Viziwi ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.
