Oct 06, 2019 23:10 UTC
  • Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 8 Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba 7 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita sawa na tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan na kufanikiwa kuuangusha utawala wa Taliban, haikuweza kumtia mbaroni Mulla Omar na viongozi wengine wa kundi hilo la Taliban.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Hussein Muhammadi Laini, faqihi mkubwa. Ayatullah Laini alizaliwa mwaka 1343 Hijiria katika moja ya vijiji vya mji wa Behshahr nchini Iran. Akiwa kijana mdogo aliondokewa na baba yake na hivyo kubakia chini ya usimamizi wa mama yake. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Najaf, Iraq ambapo aliishi kwa kipindi cha miaka 12 akisoma kwa maulama wakubwa akiwemo Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi na Mirza Hashem Amoli. Baada ya kuchukua ijaza (idhini) kadhaa za Ijtihadi na kufikia nafasi ya marjaa, alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji. Aidha Ayatullah Hussein Muhammadi Laini alishiriki katika harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala kibaraka wa Shah. Ayatullah Hussein Muhammadi Laini alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. 

Ayatullah Hussein Muhammadi Laini

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Bendera ya Ujerumani

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan.

Sohrab Sepehri

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo.