Alkhamisi tarehe 17 Oktoba mwaka 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba 17 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu SAW, Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu SAW kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Hata hivyo Mtume Muhammad (saw) alimzungumzia Uways na kumsifu licha ya kwamba hakuwahi kuonana naye. Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali (as), alishiriki kikamilifu kwenye vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya bin Abi Sufiyan na akauawa shahidi katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi Hindi. Alizaliwa mwaka 1246 Hijria nchini India na kupata elimu katika taaluma za fiqhi, Hadithi, teolojia na elimu nyingine za Kiislamu. Miir Hamid Hussein alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufunza elimu za kidini na kuandika vitabu. Kitabu muhimu zaidi cha Allamah Miir Hussein Hindi ni A'baqaatul Anwar. Vitabu vingine vya msomi huyo wa Kiislamu ni pamoja na Asfarul Anwar na Sham'ul Majalis.
Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionesha kuwa, nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.
Miaka 36 iliyopita aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vile vile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi.
Leo tarehe 17 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini Duniani. Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umaskini. Mwaka 1992 Umoja wa Mataifa uliitangaza siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.” Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa, kila mwandamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung'oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.
