Oct 19, 2019 02:36 UTC
  • Jumamosi, 19 Oktoba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria mwafaka na tarehe 19 Oktoba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala. Katika siku hii ya Arubaini pia msafara wa mateka wa Ahlul-Baiti wa Mtume uliokuwa umepelekwa Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyah uliwasili Karbala ukiwa na kichwa cha Imam Hussein na kukutana hapo na sahaba wa Mtume, Jabir bin Abdillah al Ansari na wafuasi wengine wa Imam waliokwenda hapo kufanya ziara. Siku hiyo Kichwa cha Imam Hussein kilizikwa pamoja na mwili wake. ***

Miaka 238 iliyopita katika siku kama ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha majeshi ya Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi. Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza. Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani. ***

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, alizaliwa huko katika mji wa Najaf Iraq, Ayatullah al-Udhma Mar’ashi Najafi mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Baba yake ni Sayyid Shamsuddin Mahmoud Mar’ashi aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na mafakihi wakubwa katika zama zake. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na ya utangulizi ya Kiislamu huko Najaf, Mar’ashi Najafi alianza kuhudhuria darsa na masomo ya Usul kwa Agha Dhiyau Aaraqi na Sheikh Ahmad Kashif al-Ghitaa. Akiwa na umri wa miaka 27, Ayatullah Mar’ashi Najafi alifikia daraja ya Ij’tihad. ***

Ayatullah al-Udhma Mar’ashi Najafi

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Ali Hassan Salamah mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kwa njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Salamah alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine. ***

Ali Hassan Salamah

Na miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo manowari za jeshi la Marekani zilishambulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran. Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya Kuwait iliyokuwa ikiusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran, kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa imeshambulia meli yake ya mafuta. Marekani ilivishambulia visiwa vya mafuta vya Iran kwa madai kuwa meli ya Kuwait iliyoshambuliwa na Iran ilikuwa na bendera ya nchi hiyo. ***

 

Tags