Alkhamisi tarehe 31 Oktoba mwaka 2019
Leo ni Akhamisi tarehe Pili Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe 31 Oktoba mwaka 2019
Siku kama ya leo miaka 811 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi. Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu. Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw).
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, yaani tarehe 9 Aban 1304 Hijria Shamsia, Bunge la Ushauri la Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kumuuzulu Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajar na kutangaza kuufuta kikamilifu utawala wa kizazi hicho nchini Iran kilichobaki madarakani kwa kipindi cha miaka 135. Baada ya kuondoshwa utawala wa silsila ya Qajar, Uingereza ilifanya njama za kuingilia kati na kuuweka madarakani utawala wa muda nchini ulioongozwa na Reza Khan. Reza Khan alijitangaza kuwa mfalme na kuanzisha silsila ya utawala wa Kipahlavi. Utawala huo wa Kipahlavi uliandaa mazingira ya kuporwa zaidi utajiri wa taifa na kukandamizwa wananchi wa Iran kulikofanywa na madola ya Uingereza na Marekani.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 540 baada ya utawala wa Baathi wa Iraq kushambulia meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi. Azimio hilo lilitolewa kufuatia mashambulizi ya utawala wa Iraq dhidi ya meli za kibiashara katika kipindi cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hujuma ambazo zilikuwa na lengo la kuchafua usalama wa eneo hilo. Azimio hilo lilisisitiza haki ya meli zote za kibiashara kufanya safari kwa uhuru katika maji ya kimataifa na lilizitaka nchi zote kuheshimu suala hilo. Azimio nambari 540 la Baraza la Usalama pia lilizitaka pande mbili hasimu kukomesha mapigano katika Ghuba ya Uajemi na kuheshimu ardhi ya nchi za eneo hilo. Inafaa kuashiria kuwa, azimio hilo lilitolewa huku utawala wa Saddam Hussein ukizidisha mashambulizi yake dhidi ya meli za mafuta za Iran.
Tarehe 31 Oktoba 1984 yaani siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, aliuawa Bi. Indira Gandhi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa India. Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu. Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo.
Tarehe 31 Oktoba miaka 33 iliyopita, alifariki dunia malenga wa zama hizi wa Iran, Salman Harati. Harati ambaye jina lake la asili ni Salman Qanbar Harati, alizaliwa katika kijiji cha Marz Dasht cha mji wa Tonekabon nchini Iran. Alikuwa malenga mwanamapinduzi na shakhsia wa kidini. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na ‘Asman Sabz’ na ‘Dari be Khoneh Khorshid’ kadhalika aliandika kitabu cha ‘Azin Setareh ta Ansetareh’ ambacho hufundishwa mashuleni. Alijitahidi kutumia lugha nyepesi katika mashairi yake ili kumuwia rahisi msomaji kuelewa.
Na katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, aliaga dunia Federico Fellini mtengenezaji filamu maarufu wa Kiitalia. Fellini ni miongoni mwa watengenezaji na waongozaji filamu wakubwa wa karne ya ishirini. Fellini alianza kazi ya kuandika filamu tangu mwaka 1938 na baadaye akajiingiza katika utengenezaji filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Federico Fellini akiwa msaidizi wa mtengeneza filamu aliyejulikana kwa jina la Roberto Rossellini walitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la "Rome Open City". Mwaka 1993, yaani miezi sita kabla ya kifo chake, Fellini alitunukizwa tuzo ya Oscar kutokana na kazi zake za thamani katika ulimwengu wa filamu.