Alkhamisi tarehe 7 Novemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe 7 Novemba 2019.
Siku kama ya leo tarehe 9 Rabiul Awwal miaka 1181 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wacha-Mungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo.
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuja madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi. Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia mapambano yao kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imeota kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”