Dec 16, 2019 07:16 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dec 16

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho matukio muhimu ya spoti na wanaspoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa……Karibu….

Iran bingwa wa Mashindano ya Mieleka 'Siku ya Watoto'

Timu ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika Mashindano ya Siku ya Watoto ya mchezo huo yaliyofanyika hapa nchini. Katika mieleka mtindo wa Free-style, wanamileka wa Iran wametwaa ubingwa kwa kuzoa jumla ya alama 245, wakifuatiwa na Kyrgyzstan na Azerbaijan ziliotwaa nafasi ya pili na tatu kwa alama 97 na 73 kwa usanjari huo. Aidha timu ya mileka ya Greco-Roman ya Iran imeibuka mshindi kwa kukusanya alama 235, mbele ya Kyrgyzstan na Armenia. Wanamieleka 130 kutoka Armenia, Kyrgyzstan, Azerbaijan na Turkmenistan wameshiriki mashindano hayo ya Siku ya Watoto hapa nchini, huku Iran ikiwakilishwa na timu tano.

Chesi: Muirani akataa kucheza na Mzayuni

Nyota wa mchezo wa sataranji (chesi) wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekataa kuchuana na mshindani wake wa Utawala wa Kizayuni wa Israel, ili kuonesha mshikamano na uungaji mkono wake kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina. Binti huyo wa Kiirani ambaye ni bingwa wa kimataifa anayefahamika kama Mobina Ali Nasab alijiondoa katika mchezo wake na mwakilihi huyo wa Israel, katika raundi ya tisa ya mashindano ya dunia ya mchezo huo yanayofanyika Uhuispania almaarufu Spanish International Chess Championship.

Mchezo wa sataranji au chess

 

Katika mzunguko wa nane wa mashindano hayo, mwanasataranji huyo wa kike wa Iran alimzidi maarifa hasimu wake wa India, na kumshinda kwa alama 2324 kwa 2234. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hauutambui utawala haramu wa Israel, na katika fremu ya sera zake za kimataifa, wanamichezo wa Iran huwa wanajizuia au kukataa kucheza na wachezaji wa utawala ghasibu wa Israel katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, kama njia mojawapo ya kusimama na Waislamu madhulumu wa Palestina wanaokandamizwa na ardhi zao kughsubiwa na utawala pandikizi wa Israel.

Wanasarakasi wa Iran waruhusiwa kuvaa Hijabu

Rais wa Shirikisho la Wanasarakasi Iran amesema Shirikisho la Wanasarakasi Duniani limewaruhusu wanasarakasi wa Jamhuri ya Kiislamu kuvaa vazi la staha la Hijabu wakishiriki michezo ya kimataifa. Zahra Inche Dargahi amesema Shirikisho la Wanasarakasi Duniani limefanyia marekebisho sheria zake na sasa wachezaji Waislamu wa mchezo huo wa viungo wataruhusiwa kuvaa Hijabu wanaposhiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Wanasarakasi wanaoinukia

 

Rais wa Shirikisho la Wanasarakasi Iran amebainisha kuwa, "Nilifanya mazungumzo na Nellie Kim, Naibu Rais wa Shirikisho la Wanasarakasi Duniani ili kumshawishi waruhusu uvaaji Hijabu katika kategoria zote za michezo ya sarakasi, na ninatumai kwamba ombi hilo litakubaliwa."

Soka: CECAFA (Chalenji)

Timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya, Harambee Stars, imetinga nusu fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge) na sasa itatoana jasho na Eritrea katika mechi ya nusu-fainali jijini Kampala nchini Uganda Jumanne hii ya Desemba 17. Hii ni baada ya Eritrea kujikatia tiketi ya kukutana na Kenya baada ya kumaliza Kundi A katika nafasi ya pili kwa alama tano ilipolazimisha sare tasa dhidi ya Somalia katika mechi yake ya mwisho Jumapili. Siku ya Jumamosi, Harambee Stars iliibamiza Zanzibar Heroes bao 1-0, katika mchuano wa robo fainali iliyopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Lugogo nchini Uganda. Bao hilo la kipekee la Kenya lilitiwa kimyani na mwanajeshi Oscar Wamalwa ambaye anakipiga katika klabu ya Ulinzi Stars.

Nembo za Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati

 

Nusu-fainali nyingine itakuwa kati ya Uganda, ambayo imeshinda mechi zake zote nne za makundi, na Tanzania Bara iliyokamilisha Kundi B katika nafasi ya pili. Wenyeji Uganda ilikuwa timu ya kwanza ya Kundi A kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Chalenji mwaka huu 2019, kama ilivyokuwa kwa Kenya waliopenya mapema kutoka kundi B, huku wakitamba kuwa wako tayari kukutana na wenyeji hao katika hatua yoyote. Timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' imetinga nusu fainali ya michuano ya Chalenji licha ya kumaliza sare tasa na Sudan katika mchuano wake wa Jumamosi uliopigwa katika Uwanja wa KCCA jijini Kampala.

Fainali ya michuano hiyo ya kikanda itapigwa Disemba 19. Itakumbukwa kuwa, bingwa mtetezi wa kombe hilo la Chaleji ni Kenya ambayo ilitwaa ushindi mwaka 2017 kwa kuifunga Zanzibar Heroes katika fainali iliyoisha kwa sare ya mabao 2 – 2, kabla ya kuibuka kidedea kwa penati 3 – 2. 

Riadha: Mbio za Nusu Marathon Kigali, Rwanda

Mwanariadha Marthe Yankurije ameibuka kidedea katika mbio za Nusu Marathon jijini Kigali, nchini Rwanda. Mbio hizo zilizofanyika Jumapili, Disemba 15 zimeandaliwa na Shirikisho la Riadha la Rwanda likishirikiana na Mji wa Kigali. Mwanadada huyo ambaye anaonekana kuwa nyota wa mbio za masafa marefu nchini Rwanda alikata utepe wa ushindi kwa kutumia saa moja, dakika 13 na sekunde nne, ikiwa ni dakika mbili mbele ya Adeline Musabyeyezu aliyemaliza wa pili. Katika safu ya wanaume, Yves Nimubona aliibuka mshindi wa mbio hizo za kilomita 21, kwa kutumia saa moja, daika tatu na sekunde 28. Emmanuel Mutabazi alimaliza wa pili kwa kutumia (1:03:38) huku Silogi Rubayiza ikifunga orodha ya tatu bora kwa kutumia (1:08:59). Haya yalikuwa ni mashindasno ya kwanza ya ina hiyo kufanyika tangu mwaka 2004 ambapo yalikuwepo mashindano ya Kimataifa ya Kigali Peace Marathon. Kwa mujibu wa waandaaji, zaidi ya wanariadha 2,000 wameshiriki. Mbio hizo zitatumika kama mchujo kwa wakimbiaji watakaofuzu kuiwakilisha Rwanda katika mbio za Nusu Marathon Duniani 2020 zitakazofanyika Gdynia, Poland.

Dondoo za Hapa na Pale

Bondia Mtanzania Sarafina Julius amepoteza pambano la raundi ya 10 kwa pointi dhidi ya mwanamasumbwi wa Russia Anna Levina. Pambano hilo la aina yake limefanyika jijini Moscow nchini Urusi usiku wa December 14. Pambano lilikuwa la Ubingwa IBA na WPBF. Promota wa pambano Mr Shamo kaomba marudio ya pambano hilo baada ya kuridhishwa na uwezo wa Sarafina. Haijabainika ni lini na wapi litachezwa pambano hilo la marudiano.

Mbali na hayo, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima katika masuala ya Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Laikipia nchini Kenya, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za Marathon Eliud Kipchoge ametuzwa tena Shahada ya Heshima ya Sheria wikendi hii katika Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza. Chuo hicho kimetangaza kuwa, kitamkabithi mwanariadha huyo cheti hicho wakati wa sherehe yake ya kufuzu kwa mahafali. Baraza la seneti la chuo hicho limemtambua bingwa huyo kwa ufanisi wake kwenye nyanja ya michezo. Wakati huohuo, Mfalme huyo wa mbio za Marathon amewabwaga wanaspoti mahiri duniani na kunyakua taji la BBC la kuwa Mwanaspoti Bora wa mwaka Duniani. Kipchoge amekuwa na wakati mzuri mwaka 2019, hususan alipoandika historia yake katika kivumbi cha INEOS 1:59 aliposhuhudiwa kuwa mtu wa kwanza kumaliza mbio za marathon chini ya saa mbili mwezi Oktoba. Eliud Kipchoge aliibuka kuwa chaguo bora na kunyakua taji hilo la BBC, baada ya kuzoa kura nyingi zilizopigwa kwenye mtandao.

Mwanariadha nyota wa Kenya, Eliud Kipchoge

 

Na klabu ya Arsenal ya Uingereza imejibari na matamshi ya mchezaji nyota wake, Mesut Ozil ya kuwaunga mkono Waislamu wa jamii ya Uigur wanaoandamwa na dhulma na unyanyasaji nchini China. Ozil ambaye ni Muislamu aliwaita Uighurs ''mashujaa ambao wanapinga mateso'' na kuikosoa China pamoja na idadi kubwa ya Waislamu waliolifumbia macho jambo hilo. Klabu hiyo imetuma taarifa kwa vyombo vya habari ambayo sehemu yake moja inasema, ''Kufuatia ujumbe katika mitandao ya kijamii kutoka kwa Mesut Ozil, klabu ya Arsenal lazima iweke wazi kwamba hayo ni maoni ya kibinafsi ya Mesut.'' Usimamizi wa Gunners umesema ''Arsenal haipendi kujihusisha katika maswala ya kisiasa kama shirika.'' Shirika la Soka nchini China lilisema kwamba matamshi ya Ozil 'hayakubaliki' na yameumiza hisia za wafuasi wengi wa China. Kadhalika kanali ya CCTV ya Shirika la Utangazaji la China ilikataa Jumapili kurusha hewani mchuano kati ya Arsenal na Manchester City, kulalamikia kauli hiyo ya Ozil. Gunner waligaragazwa mabao 3-0 katika mchuano huo licha ya kuupigia nyumbani Emirates.

Ozil na Rais Erdogan wa Uturuki

 

Makundi ya haki za kibinadamu yanasema kwamba karibia watu milioni moja wengi wao kutoka kwa jamii ya Uighur walio Waislamu wanadaiwa kuzuiliwa bila kufunguliwa mshtaka katika kambi moja ya jela. Hata hivyo China inasema kwamba Waislamu hao wanapatiwa mafunzo katika kambi ili kukabiliana na ghasia na itikadi kali za kidini. Wachambuzi wa mambo wameikosoa klabu ya Arsenal kwa kutosimama na mchezaji wake, hatua ambayo wengine wanaweza kutafsiri kuwa wanaunga mkono upande wa pili, yani upande wa dhulma na ukandamizaji.

……………………..TAMATI…………….….