Feb 15, 2020 08:51 UTC

Assalaamu Alaykum Wapenzi Wasikilizaji wa Radio Tehran, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale mlipo. Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kipya cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki juma lililopita tulizungumzia kwa muktasari jinsi Maulama na wanazuoni wa dini walivyo nafasi na daraja ya juu katika utamaduni wa Kiislamu. Tulikunukulieni hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (saw) inayosema kuwa, Maulamaa ni warithi wa Mitume. Aidha tulisema kuwa, wanazuoni na wenye elimu wametajwa katika Qur'ani baada ya Mwenyezi Mungu na Malaika kwamba ni mashuhuda ya kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Sehemu hii ya pili ya kipindi hiki itamtambulisha Sheikh Kulayni alimu na mwanazuoni mashuhuri zaidi wa Kishia katika zama za Ghaiba Ndogo (Ghaibat al-Sughra). Natumai mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache za kipindi hiki.

Sheikh Kulayni

 

Sheikh Kulayni ambaye alijulikana baina ya watu kwa ukweli wa maneno na matendo alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na riwaya, kiasi kwamba, Mashia kwa Masuni walikuwa wakimtambua kama marejeo yao ya utafiti wa kidini. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akawa akitambulika kwa lakabu ya Thiqat al-Islam yaani mtu mwenye kuaminika katika Uislamu. Sheikh Kulayni ndiye mtunzi wa kitabu cha al-Kafi, moja ya vitabu muhimu na vyenye thamani kubwa katika majimui ya vitabu vinne vya hadithi vya Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kama Kutub al-Ar'baa.

Sheikh Abu Ja'far Muhammad ibn Ya'qub Ibn Ishaq al-Kulayni al-Razi ni mwanazuoni mkubwa na fakihi mashuhuri wa Kishia katika karne ya tatu Hijria. Kwa mujibu wa nyaraka za historia zilizopo, alizaliwa mwaka 258 Hijria katika kijiji cha Kulayl katika viunga vya mji wa Rey moja ya miji mikongwe ya Iran. Familia yake ilikuwa mashuhuri kwa elimu na kushikamana na dini na alizaliwa katika zama ambazo zilisadifiana na kipindi cha Uimamu wa Imam Hassan Askary (as) Imam wa 11 katika mlolongo wa Maimamu 12 wa nyumba ya Bwana Mtume (saw). Baba na mjomba Sheikh Kulayni walikuwa wasomi na wanazuoni weledi na watajika wa hadithi katika zama zao. Sheikh Kulayni aliaga dunia katika zama za kumalizika kipindi cha Ghaibat al-Sughra yaani mwaka 329 Hijria. Kwa msingi huo alifanikiwa kuishi katika kipindi cha Manaibu na wawakilishi wanne wa Imam Mahdi (atfs) na hivyo kupata fursa ya kuwasiliana kwa uchache na manaibu maaluumu wa Imam Mahdi (as).

Awali Sheikh Kulayni alisoma masomo ya msingi ya Elimu za Kiislamu kwa baba na mjomba wake. Baada ya hapo akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alielekea katika mji wa Rey. Katika zama hizo, licha ya kuwa, mji wa Rey ambao kijiografia ni moja ya miji ya Iran, wakazi wake wengi walikuwa wafuasi wa madhehebu ya Shafi na Hanafi, lakini wakazi wa vijijini walikuwa Mashia waliokuwa na mapenzi makubwa na Ahlul-Baiti (as) ambapo heshima, tabia yao njema na miamala yao mizuri ilipelekea watu wengine wawaheshimu na kuwathamini.

 

 

Kwa muktadha huo mji wa Rey ukafahamika kuwa wa Mashia. Akiwa mjini Rey Sheikh Kulayni alisoma elimu ya hadithi kwa Abul-Hassan Muhammad bin Asadi Kufi. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Sheikh Kulayni alihajiri na kuelekea katika mji wa Qum ambapo akiwa huko alikutana na watu waliopokea hadithi moja kwa moja kutoka kwa Imam Hassan Askary (as) au Imam Hadi (as) na kusoma pia kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Baadaye alihajiri katika mji huo na kuelekea mjini Kufa Iraq. Katika zama hizo mji wa Kufa ulikuwa moja ya vituo vikubwa vya kielimu ambapo wasomi wakubwa walikuwa wakielekea katika mji huo kwa ajili ya kufanya tablighi na itikadi zao kwa uhuru kamili.

Safari ya kielimu ya Sheikh Kulayni haikuishia hapo kwani baadaye alielekea Baghdad. Akiwa huko alipata umashuhuri mkubwa kiasi kwamba, Mashia na Masuni walikuwa wakimrejea kwa ajili ya mambo mbalimbali ya kidini yaliyowatatiza, na fatuwa zake zilikuwa zikiaminiwa na makundi yote hayo mawili. 

Sambamba na kipindi cha Ghaibat al-Sughrah ya Imam Mahdi (atfs) watu walikosa neema ya uwepo wa Imam Maasumu. Katika zama hizo, baadhi ya watu walikuwa wakifanya njama za kupachika hadithi za uongo au kupotosha hadithi zilizokuweko, wakitumia vibaya anga ya kutokuweko Imam Maasumu, hivyo walikuwa wakikusanya wafuasi ili kufikia malengo yao binafsi.

Kitabu cha al-Kafi

 

Kwa kuzingatia kwamba mji wa Rey katika zama hizo ulikuwa moja ya miji muhimu ya Kiislamu, kulikuweko na makundi mbalimbali ya Kiislamu ambayo nayo yalikuwa yakifanya juhudi za kuwa na udhibiti na ushawishi katika mji huo. Hali hiyo ilipelekea kujitokeza ushindani mkubwa na wa ajabu baina ya madhehebu mbalimbali ya Kiiislamu.

Katika mazingira kama haya, Maulamaa na wanazuoni wa dini kutoka katika madhehebu mbalimbali za Kiislamu walifanya hima na idili kubwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, hazina na dafina ya hadithi na riwaya inahifadhiwa. Mazingira hayo yalipelekea kipindi hicho kitambulie kama "Zama za Hadithi". Ni katika zama hizo pia vitabu sita mashuhuri vya Kisuni vinavyojulikana kwa jina la Sihah Sittah yaani Sahihi Sita vilipoandikwa.

 

Sheikh Kulayni ambaye aliishi katika zama za Ghaibat al-Sughra aliweza kutambua vyema hitajio hasa la zama hizo na kwa kuwa alikuwa akidiriki vyema hatari ya dini kupotoshwa, alichukua uamuzi wa kukusanya hadithi na maarifa ya Ahlul-Baiti (as) ili kupitia maagizo na maelekezo ya Maasumina, watu waweze kuokoka na upotofu. Baada ya kukata shauuri la kukusanya hadithi, Sheikh Kulayni alianza kufanya safari katika miji na maeneo mbalimbali ya Kiislamu na kuanza kufanya kazi hiyo iliyomchukulia muda na wakati mwingi.

Kaburi la Sheikh Kulayni huko Iraq

 

Katika zama za Sheikh Kulayni mbali na watu wa kawaida, maulama na wanazuoni pia walikuwa chini ya mashinikizo makubwa. Kutokana na kutokuweko Imam Maasumuu, watu hawakuwa na chemchemi ya elimu na hekima na kwa upande mwingine hakukuweko na chanzo kingine cha kuaminika ili waweze kukitumia kwa ajili ya kutoa majibu ya maswali ya mambo na hukumu tofauti za dini. Hivyo basi hata Maulamaa hawakuwa na uwezo wa kutoa majibu ya maswali mengi.

Baada ya juhudi na hima ya miaka kadhaa iliyoambatana na taabu na mashaka mengi, hatimaye Sheikh Kulayni alifanikiwa kuwapatia Waislamu na Maulamaa wa dini kitabu chenye thamani kubwa cha al-Kafi. Hii leo baada ya kupita zaidi ya miaka 1000 hakuna alimu, mtafiti na msomi wa madhehebu yoyote ambaye anaweza kudai kwamba, hakihitajii kitabu hiki.

Kipindi chetu kijacho juma lijalo kitaendelea kubainisha zaidi maisha ya Sheikh Kulayni pamoja na kitabu chake cha al-Kafi. Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kukunukulieni hadithi kutoka kwa Amirul-Muumina Ali bin Abi Twalib (as) ambaye amenukuliwa akisema: Alimu yuko hai hata kama amekufa, na mjinga ni mfu hata kama yuko hai.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.