Alkhamisi 12 Machi, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Rajab mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Machi mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 170 iliyopita alizaliwa Ayatullahil Udhma Sayyid Abu-Turab Khansari, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu huko Khansar, moja ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullahil Udhma Khansari alipata elimu kwa maustadhi muhimu wa zama zake. Juhudi zake masomoni zilimfanya aondokee kuwa ustadhi mahiri katika masomo ya fiqhi, usulul fiqhi na tafsiri ya Qur'ani. Ayatullah Khansari ameandika vitabu vingi kuhusiana na elimu mbalimbali za kidini. Kitabu cha Qasdus Sabil kuhusiana na elimu ya usulul fiqhi na Misbahus Swalihiin kinachozungumzia misingi ya dini, ni baadhi tu ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyu mahiri wa Kiislamu aliyefariki dunia mwaka 1346 Hijria.
Miaka 166 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkataba wa kihistoria wa Constantinople (Istanbul) ulitiwa saini baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala wa kifalme wa Othmaniyyah. Baada ya nchi hizo tatu kutia saini mkataba huo dhidi ya sera za kujitanua za Urusi ya zamani huko Ulaya, zilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata ushindi dhidi ya Urusi katika vita vya Crimea.
Miaka 95 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China. Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi. Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China.
Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Esfand 1358 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini MA alitoa amri ya kuundwa taasisi ambayo itakuwa ikishughulikia hali za familia za mashahidi waliouawa wakitetea Mapinduzi ya Kiislamu nchini. Taasisi hiyo hadi sasa bado inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi kwa familia za mashahidi wa harakati za mapinduzi na hali kadhalika familia za mashahidi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.
