Jumapili, tarehe 7 Juni, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 15 Shawwal 1441 Hijria, sawa na tarehe 7 Juni 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1189 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (as). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt (as) kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.
Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita sawa na tarehe 15 Shawwal 1248 Hijiria, alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".
Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita, Paul Gauguin, mchoraji mashuhuri wa Kifaransa alizaliwa mjini Paris. Alipata hamu ya uchoraji kutoka kwa mke wake ambaye alikuwa mwalimu wa uchoraji. Hatimaye aliamua kusafiri hadi katika kisiwa cha Tahiti kilichoko katika bahari ya Pacific ili kuendeleza sanaa hiyo. Akiwa katika kisiwa hicho alichora picha za kuvutia kuhusiana na mazingira na pia maisha ya watu wa kisiwa hicho hadi alipofariki dunia mwaka 1903.
Siku kama hii ya leo miaka 141 iliyopita, yaani sawa na tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na suala hilo liliifanya Chile iishambulie kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita na kufuatia kushindwa Waarabu katika vita na utawala haramu wa Israel, askari wa utawala huo waliingia katika mji wa kihistoria na kidini wa Baitul Muqaddas. Waislamu wanaupa utukufu maalumu mji huo kutokana na kuwa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu unapatikana humo na pia kutokana na kuwa ni sehemu ambayo Mtume Mtukufu (saw) alipaa kuelekea mbinguni katika tukio la Mi'raaj kutokea hapo. Tangu utawala ghasibu wa Israel uzikalie kwa mabavu ardhi za Wapalestina, umekuwa ukitekeleza njama hatari za kuuharibu msikiti huo na badala yake kujenga hapo hekalu bandia la Nabii Suleiman (as). Utawala huo vilevile unatekeleza siasa hatari ya kuvuruga muundo wa jamii asili ya wakazi wa mji wa Baitul Muqaddas kwa kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kujenga hapo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni. Walowezi hao wa Kizayuni wanafanya njama kubwa ya kufuta kabisa nembo na alama za Wapalestina na Waislamu katika mji huo mtukufu wa Baitul Muqaddas.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya shambulizi hilo kuharibu kikamilifu kituo hicho cha nyuklia na kuzikasirisha fikra za waliowengi duniani na vilevile kulaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hakuna hatua yoyote ya kivitendo ilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia.