Jun 14, 2020 02:41 UTC
  • Jumapili, Juni 14, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 14 mwaka 2020 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 290 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Muhammad Hussein Khatunabadi aliyekuwa alimu na msomi mkubwa wa Kiirani. Alikuwa hodari katika fiqhi, fasihi na elimu ya hadithi na alikusanya na kuandika hadithi nyingi za Mtume (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni "Al Alwahu al Samaawiyyah" na "Al Najmu al Thaqib". 

Ayatullah Muhammad Hussein Khatunabadi

Siku kama ya leo miaka 284 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina Lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Charles Augustin de Coulomb

Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kulikomboa eneo hilo.

Sudan

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili, kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za walio wengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha. Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China. Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika.

Mto wa Yangtze Kiang

 

  Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 Miladia nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama vile Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges akaanza shughuli ya uandishi na taratibu akaanza kuandika kisa mashuhuri cha Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu wake, hakuweza kumaliza kuandika kisa hicho. Luis ameacha athari mbalimbali za vitabu ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.

Jorge Luis Borges