Jul 17, 2020 21:59 UTC
  • Jumamosi, 18 Julai, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 18 Julai 2020.

Siku kama ya leo miaka 1149 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9. Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896. ***

Uingereza na Denmark

 

Miaka 239 iliyopita katika siku kama ya leo, William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia. Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo. Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.***

William Herschel

 

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita,  Zuheir Muhsin, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya al Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa mashirika ya ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) na lile la Misri huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Maajenti wa tawala hizo mbili walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo. Zuheir Muhsin alikuwa mpinzani mkubwa wa mapatano ya kisaliti ya Camp David na aliwahi kutishia mara kadhaa kwamba harakati yake ya al Sa'iqa itamuua mtawala wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadaat aliyetia saini makubaliano hayo na Wazayuni. ***

Zuheir Muhsein,

 

Na Tarehe 18 Julai, ni "Siku ya Kimataifa ya Mandela". Mwaka wa 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku hii kuwa siku mahsusi kwa Nelson Mandela, mwasisi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Umoja wa Mataifa uliitangaza siku ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, yaani tarehe 18 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ya Mandela ili kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati ya kupigania uhuru nchini Afrika Kusini na juhudi zake kubwa za kutangaza amani, kutilia maanani utatuzi wa migogoro baina ya kaumu na nchi mbalimbali, kutetea haki za binadamu, na kuwepo usawa na maelewano baina ya wanadamu wa mbari na kaumu zote. Mandela alifariki dunia tarehe 5 Disemba mwaka 2013. ***

Hayati Nelson Mandela