Jumatatu tarehe 20 Julai 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Pili Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 20 mwaka 2020.
Tarehe 28 Dhilqaada miaka 1081 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya hadithi za Mtume (saw). Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya utafiti na uchunguzi wa miaka 33.
Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya hadithi kwa majina ya Al Muujamul Kabiir", al Muujamul Wasiit na al Muujamus Swaghir.

Miaka 210 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 Miladia, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi.

Katika siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati.
Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, kulifanyika maandamano makubwa mjini Tehran na kwenye miji mingine ya Iran baada ya Dakta Musaddiq kujiuzulu cheo cha Waziri Mkuu. Wakati huo Ayatullah Kashani alitoa taarifa ya maneno makali baada ya Dakta Musaddiq aliyekuwa Waziri Mkuu kujizulu na Shah kumteuwa Ahmad Qavam mashuhuri kwa jina la Ghavam Sultaneh kuwa Waziri Mkuu. Ayatullah Kashani alitoa taarifa hiyo akilalamikia vikali agizo la Shah la kumteuwa Ghavam kushika wadhifa huo. Ahmad Qavam ambaye alikuwa na uhusiano na wakoloni na kibaraka wa utawala wa kibeberu wa wakati huo, muda mfupi baada ya kuwa Waziri Mkuu, alianzisha njama za kutenganisha dini na siasa na kuendesha propaganda dhidi ya Ayatullah Kashani na wanaharakati wa Kiislamu nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.
Na miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo.