Aug 12, 2020 02:32 UTC
  • Jumatano tarehe 12 Agosti mwaka 2020

Leo ni Jumatano tarehe 22 Dhulhija 1441 Hijria inayosadifiana na Agosti 12 mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). 

Mahali lilipo kaburi la Maitham Tammar

Siku kama ya leo miaka 960 iliyopita alifariki dunia malenga na arifu mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria, Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama hii ya leo miaka 44 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati. Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon. 

Mauaji ya Wapalestina katika kambi ya Tel al Zaatar  

Na miaka 21 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa. Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia. Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukzia vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili. Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbali zinazolikabili tabaka hilo muhimu.