Sep 21, 2020 18:54 UTC
  • Jumatatu tarehe 21 Septemba 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 3 Safar 1442 Hijria sawa na Septemba 21 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1832, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha.

Sir Walter Scott

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, yaani 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkurumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.

Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.

Shambulizi la Saddam dhidi ya Saddam Hussein

Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.

Marufuku ya vazi la hijabu nchini Ufaransa

 

Tags