Dec 22, 2020 05:02 UTC
  • Jumanne, 22 Desemba, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 7 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 22 Desemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2166 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania.***

Duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma

 

Miaka 381 iliyopita  katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699 Miladia.***

Jean Racine

 

Katika siku kama ya leo miaka 327 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile. ***

Zilzala

 

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Kanali ya Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Kanali ya Suel, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri ya kutangaza kutaifisha kanali hiyo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo, na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.***

Bandari ya Port Said mwaka 1880

 

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo  ya tarehe 7 Jamadil Awwal Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani Tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al-Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa katika harakati za kisiasa nchini Misri. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Sayyid Qutb alikuwa akiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapamban huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa". ***

Sayyid Qutb

 

Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989 Miladia, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa. Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.

Nicolae Ceausescu,