Jan 09, 2021 11:03 UTC

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki.

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kutupia jicho kwa mukhtasari maisha ya Said bin Abdallah Ravandi Kashani mashuhuri kwa jina la Qutub Ravandi msomi, alimu, mpokezi wa hadithi, mwanateolojia, fakihi, mwanafalsafa na mwanahistoria mkubwa wa Kishia aliyeishi katika karne ya sita Hijria. Tulieleza kwamba, alimu na msomi huyo alikuwa mmoja wa wanafunzi hodari na maalumu wa Sheikh Tabarsi ambaye ni mwandishi wa Tafsiri ya Qur’ani ya Majmaul-Bayan. Aidha tulitaja na kuashiria baadhi ya vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo kama Tahaafatul Falasifa, Tafsirul-Qur’ani wa Taawil al-Ayaat na Kharaij wa Jaraih. Katika sehemu hii ya 17 wiki hii, tutaangazia kwa mukhtasari historia na maisha ya Ibn Shahr Ashoub, alimu na msomi mwingine wa Kiislamu aliyeishi katika karne ya sita Hijria. Karibuni.

 

Muhammad bin Ali bin Shahr Ashoub mashuhuri kwa jina la Ibn Shahr Ashoub alizaliwa katika mwezi wa Jamadu Thani mwaka 488 Hijria. Familia yake ilikuwa na asili ya mji wa Sari huko Mazandaran Iran. Kwa maneno mengine ni kuwa, familia yake ilikuwa na asili ya Ukingo wa Kusini mwa Bahari ya Caspian. Hata hivyo baba na babu yake walikuwa wakiishi Baghdad, Iraq. Kuna hitilafu baina ya wanahistoria kuhusiana na mahala hasa alipozaliwa Ibn Shahr Ashoub, je ni Baghdad, Iraq au ni Sari nchini Iran.

Mahala lilipo kaburi la Ibn Shahr Ashoub

 

Baba yake Ibn Shahr Ashoub aliyeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sheikh Ali alikuwa mmoja wa wanazuoni mahiri na stadi wa fikihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mkubwa katika Ulimwengu wa Kishia. Mwanazuoni huyu alifanya hima na juhudi kubwa katika kuwalea watoto wake.  Kutokana na malezi mema ya baba yake, Muhammad alifanikiwa kuwa na malezi bora na ufahamu mkubwa. Akiwa na umri wa miaka 8 Ibn Shahr Ashoub alikuwa amehifadhi kwa moyo Qur'ani yote. Tabia yake njema na uzuri wa maneno ni mambo ambayo yaliwavutia mno watu wa karibu yake.

Mapenzi, hamu na shauku kubwa ya Ibn Shahr Ashoub ya kujifunza na ari pamoja na hima aliyokuwa nayo ya kutafuta elimu, ni urithi mkubwa alioupata kutoka kwa baba yake aliyeondokea kuwa mashuhuri kwa wema, tabia njema, uchaji Mungu na elimu.

Kile ambacho kilimsadia mno Muhammad katika njia ya kupokea ukweli na kumpeleka mbele katika njia ya ukamilifu ni riziki ya halali ambayo ilikuwa ikiletwa nyumbani na baba kwa ajili ya familia yake. Mafundisho ya Kiislamu  yamesisitiza mno juu ya taathira chanya na nzuri ya chakula cha halali katika kumpa tawfiki mtu ya kufikia ukamilifu na maadili mema.

 

Kaburi la Ibn Shahr Ashoub

 

Baada ya kusoma Qur’ani na masomo ya msingi alianza kujifunza kwa bidii kubwa elimu na maarifa ya Kiislamu kama fikihi, usulul fikih, hadithi, teolojia tafsiri ya Qur’ani na kadhalika. Maulamaa wakubwa kama Sheikh Tabarsi na Qutub al-Ravandi walikuwa miongoni mwa walimu wake.

Ibn Shahr Ashoub aliweza kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali vya kidini (Hawza) nchini Iran na kufanya safari mbalimbali za kielimu katika miji ya Iran kama Qum, Rey, Mash’had, Kashan, Neishbaour, Isfahan na Hamadan. Katika safari zake hizo, msomi huyu alinufaika na bahari ya elimu ya wanazuoni na maulama wakubwa wa zama hizo katika miji hiyo.

Baadaye Ibn Shahr Ashoub alihajiri na kuelekea katika mji wa Baghdad huko Iraq. Katika zama hizo, Baghdad ulikuwa mji mkuu wa Bani Abbas na kituo mashuhuri zaidi cha elimu za Kiislamu ambapo wasomi na wanazuoni wakubwa walikuwa wakijishughulisha na kufundisha na kufanya uhakiki. Baada ya muda Ibn Shahr Ashoub alihajiri na kuelekea katika mji wa Hilli huko huko Iraq ambapo baada ya kuishi kwa miaka mingi katika mji huo alikata shauri kuhamia katika mji mwingine wa Iraq wa Mosul. Baadaye alielea huko Halab Syria na kuishi huko hadi mwishoni mwa umri wake. Katika zama hizo mji wa Halab ulikuwa makazi ya akthari ya shakhsia wakubwa na wakazi wa mji huo walikuwa na muamala mzuri na Mashia na walikuwa wakiwatukuza na kuwathamini wanazuoni wa Kishia.

Licha ya kuwa katika zama alizoishi Ibn Shahr Ashoub kulikuweko na wanazuoni na wasomi wakubwa ambao walikuwa na hadhi na itibari mbele ya Waislamu na walikuwa wakiheshimiwa mno, lakini alimu huyu alikuwa na umashuhuri wa aina yake na alikuwa na daraja ya juu ya kielimu. Kila mahala miongoni mwa ardhi za Kiislamu alizokuwa akifanya safari, Ibn Shahr Ashoub alikuwa akipokewa na shakhsia wakubwa wa maeneo hayo. Aliweza kutumia elimu yake kufundisha na kulea wanafuzni ambapo baadaye waliondokea kuwa wanazuoni mahiri.

Picha ya kale ya mwaka 1962 ya kaburi la Ibn Shahr Ashoub katika mji wa halab

 

 

Ibn Shahr Ashoub alitambulika na kusifika mno kwa unyenyekevu, ukweli na ufasaha katika uzungumzaji. Mbali na harakati za kufundisha Ibn Shahr Ashoub alikuwa akialifu vitabu sambamba na kutoa mawaidha.

Moja ya sifa zilizomfanya Ibn Shahr Ashoub aonekane yuko juu ikilinganishwa na maulamaa wengine wa zama zake ni insafu na uadilifu pamoja na mitazamo yake ya kielimu kuwa yenye thamani. Sifa hii na fatuwa zake zilizokuwa na mashiko na hoja madhubuti ni mambo yaliyowafanya hata wanazuoni wa Kisuni kumsifia na kumtaja kwa wema.

Ktabu cha manaqib Aal Abi Talib, ndio kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Shahr Ashoub ambacho hadi sasa kimechapishwa mara kadhaa. Kitabu hiki ni mjumuiko wa historia ya maisha na fadhila za Maasumina 14 yaani Bwana Mtume SAW, Bibi Fatma Zahra AS na Maimamu kumi na mbili kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW. Kitabu chake kingine ni Maalimu al-Ulamaa ambacho licha ya kuwa ni kidogo lakini kina thamani kubwa mno. Aidha Ibn Shahr Ashoub ana kitabu kingine kiitwacho Mutashabihil Qur’an wa Mukhtalifuh.

Hatimaye Ibn Shahr Ashoub aliaga dunia usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarene 22 ya mwezi Shaabah 588 Hijria huko Halab Syria akiwa na umri wa takriban miaka 100. Hii leo, upepo mwanana wa maarifa ya Ahlul-Baiti AS pamoja na urithi wa elimu ya mwanazuoni huyo unapepepea taratibu na kuwafikia watafuta haki kote ulimwenguni. Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa hadithi ya Imam Ali bin Abi Talib AS ambapo amenukuliwa akisema: Alimu yu hai hata akiwa amekufa, mjinga ni mfu hata akiwa yu hai.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.