Jan 24, 2021 02:36 UTC
  • Jumapili, 24 Januari, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 10 Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 24 Januari 2021.

Miaka 815 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa arifu na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa mwaka 513 Hijria Qamaria katika eneo la Naishabur na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu na kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo.

Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantiqu Twair."

 

Siku kama ya leo miaka 354 iliyopita, Mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.

Katika siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani. Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

Kisima cha kwanza cha mafuta

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Winston Churchill

Na Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, licha ya kuwa utawala wa Shah hapa Iran ulikuwa umepiga marufuku mkusanyiko wa zaidi ya watu wawili katika miji mingi hapa nchini, lakini matabaka mbalimbali ya wananchi yalipuuza monyo ya serikali ya kijeshi dhidi ya maandamno na kuendelea kufanya maandamano. Vibaraka wa utawala wa Mfalme Shah walitumia mabavu na ukandamizaji mkali, ingawa hawakufanikiwa kuwadhibiti wananchi. Ukatili na utumiaji mabavu wa maafisa usalama dhidi ya wananchi ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya wananchi katika miji mbalimbali ya Iran. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la anga walijitokeza katika barabara za Tehran na kuandamana dhidi ya utawala wa Shah na kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini (MA).