Jan 25, 2021 02:34 UTC
  • Jumatatu tarehe 25 Januari 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 11 Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 25 Januari 2021.

Siku kama ya leo miaka 1044 iliyopita aliaga dunia mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga wa Kiirani, Badiu Zaman al Hamdani. Alizaliwa huko Hamedan magharibi mwa Iran na kupata umashuhuri kwa jila la Fadhil Hamedani. Badiu Zaman alibobea sana katika kuandika mashairi na nathari kwa lugha ya Kiarabu na alikuwa hodari mno katika utungaji wa mashairi. Miongoni mwa vitabu vya malenga huyo wa Kiirani ni Rasaailu Badiu Zaman.

 

Miaka 565 iliyopita katika siku kama ya leo, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. 

Sekta ya uchapishaji

 

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Norway kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani. 

Hansen

Miaka 15 iliyopita katika siku kama ya leo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla ya viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba ingeunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.

Nembo ya Hamas

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, duru ya Uwaziri Mkuu wa Amir-Abbas Hoveyda  mmoja wa shakhsia waliokuwa watiifu kwa utawala wa Kifalme wa Shah hapa Iran ilianza. Baada ya kunyongwa Hassanali Mansour, Waziri Mkuu wa wakati huo wa  utawala wa Shah, Amir-Abbas Hoveyda aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Baraza la Mawaziri la Mansour aliamriwa kuunda serikali akiwa Waziri Mkuu. Amir-Abbas Hoveyda alishikilia wadhifa huo kwa takribani miaka 13 yaani hadi mwaka 1977. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifo kutokana na jinai alizotenda.

Na Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, kundi lililokuwa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu lililojulikana kwa jina la Muungano wa Wakomonisti, lilishambulia mji wa Amol wa kaskazini mwa Iran. Kundi hilo lilikuwa likijidanganya kwamba, eneo hilo lingekuwa kituo cha mashambulio yake ya baadaye kaskazini mwa Iran. Vikosi vya wapiganaji na wananchi wanamapinduzi wa mji huo kwa muda mfupi walifanikiwa kuzima mashambulio ya kundi hilo lililokuwa dhidi ya mapinduzi. Kusimama kidete mtaa kwa mtaa kwa wananchi wa mji wa Amol dhidi ya mashambulio ya kundi hilo kuliufanya mji wa Amol utambulike na kuwa mashuhuri kwa jina la mji wa ngome elfu moja.

Waasi katika eneo la Amol