Jan 28, 2021 02:33 UTC
  • Alkhamisi, 28 Januari, 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Mfunguuo Tisa Jamadithani 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 28 Januari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 937 aliyopita, alifariki dunia msomi na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiiran Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Baada ya kuaga dunia baba yake, yeye na kaka yake, Ahmad walilelewa na Ahmad bin Radkani. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo ili aende mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme." ***

Imam Muhammad ghazali

 

Katika siku kama ya leo miaka 130 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Habibullah Rashti, mmoja wa maulama na maraajii wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Katika kujiendeleza kielimu, alifunga safari kuelekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Sheikh Mortadha  Ansari ambapo taratibu alikwea marhala za kielimu na hata kufikia umarjaa wa kidini. Kitabu cha 'Badaaiul-Afkaar' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo. ***

Ayatullah Mirza Habibullah Rashti

 

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya vikosi vya Uingereza na Umoja wa Kisovieti kuivamia Iran tarehe 20 Shahrivar mwaka 1320 Hijria Shamsia, kukatiwa saini makubaliano ya pande tatu baina ya nchi hizo. Kwa mujibu wa mkataba na makubaliano hayo, serikali ya wakati huo ya Iran ikawa haina budi ghairi ya kukubali kuruhusu njia zake za mawasiliano za ardhini, angani na majini kwa ajili ya nchi waitifaki ili zitumie njia hizo kwa ajili kuipelekea suhula kambi ya Umoja wa Kisovieti iliyokuwa ikipigana dhidi ya Ujerumani ya Kinazi. ***

Vita vya Pili vya Dunia

 

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita sawa na tarehe 9 Bahman mwaka 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, watu wengi wa mji wa Tehran walielekea katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya wanaharakati wa kidini kukusanyika katika chuo hicho wakipinga hatua ya utawala wa Shah ya kumzuia Imam Khomeini (M.A) kurejea nchini. Wananchi waliandamana katika miji mingine ya Iran kupinga hatua hiyo na kutaka kupinduliwa utawala wa kidhulma wa Shah na kurejea Imam Khomeini (M.A) nchini. Siku hiyo wanajeshi wa utawala wa Shah kwa mara nyingine waliwashambulia wananchi na kujeruhi na kuua shahidi Waislamu wengi miongoni mwao. ***

Mgomo wa kuketi chini masheikh katika Chuo Kikuu cha Tehran

 

Na siku hii ya leo, yaani tarehe 28 mwezi Januari, inaadhimishwa duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuwasaidia Wagonjwa Wenye Maradhi ya Ukoma. Siku hii ilipewa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa yapata nusu karne iliyopita. Wakati huo dunia ilikuwa na watu milioni 15 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliiainisha tarehe 28 Januari kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma. Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ukoma  waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kikamilifu. ***

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma