Feb 04, 2021 02:44 UTC
  • Alkhamisi, 4 Februari, 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Mfunguo Tisa Jamadithani mwaka 1442 Hijria mwafaka na tarehe Nne Februari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1058 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Jamaduth-Thani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu. Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi ya mashairi. Aidha kwa muda mfupi Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kisha akajishughulisha na kazi ya ukadhi. Kitabu cha ‘Faraj baada sh-Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Aidha kati ya vitabu vyake vingine ni kitabu cha ‘Al-Masaajid’ ambacho kinazungumzia kwa kiasi kikubwa masuala ya akhlaqi.***

محسن بن علی تنوخی

 

Miaka 333 iliyopita sawa na tarehe 4 Februari mwaka 1688 Miladia, Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa. Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo. Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne. ***

Pierre Marivaux

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika Peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani kufuatia kubainika sababu za kushindwa wazi Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Mkutano huo uliwakutanisha pamoja  viongozi wa nchi za Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya zamani (Churchill, Roosevelt and Stalin). Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki. **** 

Kuanzia kushoto kwenda kulia,
Stalin, Roosevelt na Churchill huko Yalta  

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948.***

Bendera ya Srilanka 

Na miaka 5 iliyopita sawa na tarehe 4 Februari mwaka 2016 aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri. Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa tayari amehifadhi Qur'ani nzima katika rika la ubalobaro na kuanza kusoma kitabu hicho katika hafali na majlisi mbalimbali akiwa na umri wa miaka 16. Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran. Qiraa na kisomo cha gwiji huyo wa Misri kilipendwa sana nchini Iran. Hatimaye Qarii huyo mashuhuri aliaga dunia alfajiri ya Alkhamisi tarehe 4 Februari mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kuugua kwa muda mrefu.***

Raghib Mustafa Ghalwash

 

Tags