Feb 13, 2021 02:52 UTC
  • Jumamosi, 13 Februari, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi ya mwezi Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 13 Februari 2021 Miladia.

Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 1079 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Nu'uman bin Muhammad Tamimi, alimu na mwanazuoni stadi wa Morocco aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijria. Nu'uman awali alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Maliki, kisha baadaye akajiunga na kuundi lililokuwa limedhihiri la Shia Ismailia. Baadaye akaondokea kuwa mtungaji wa sheria wa kundi hilo. Nu'uman bin Muhammad alipewa vyeo na nyadhifa muhimu katika zama za makhalifa na watawala wa Kifatimiya.  Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Daaimul Islam, Sharhul Akhbar na Tawhid wal-Imamah. ***

Nu'uman bin Muhammad Tamimi

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini alitoa fatuwa iliyomtambua Salman Rushdie, mwandishi wa kitabu cha "Aya za Shetani" au Satanic Verses kuwa ameritadi na kutoka katika dini ya Kiislamu. Katika kitabu hicho Rushdie alimvunjia heshima na kudhalilisha Mtume Muhammad (saw), kitabu kitukufu cha Qur'ani na matukufu mengine ya Kiislamu. Uandishi na uchapishaji wa kitabu hicho ulifanyika kwa njama na msaada wa nchi za Magharibi. Hata hivyo fatuwa ya Imam Khomeini dhidi ya murtadi Salman Rushdie, iliwaamsha Waislamu na kuwatahadharisha kuhusu njama hiyo. Fatuwa hiyo ya Imam iliungwa mkono na waandishi wengi huru duniani, maulamaa wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC.***

Murtadi Salman Rushdie,