Feb 13, 2021 23:05 UTC
  • Jumapili tarehe 14 Februari 2021

Leo ni Jumapili tarehe Pili Rajab 1442 Hijria Sawa na Februari 14 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1221 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria,  alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq. Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria. 

Ibn Rumi

Katika siku kama ya leo miaka 1002  iliyopita, alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale. Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa. 

Abu Raihan Biruni

Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni waliokuwa na silaha na wanachama wa kundi la kigaidi la Palmach waliendeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Palestina kwa kutekeleza shambulizi la kigaidi dhidi ya wakazi wa kijiji cha Sa'sa' huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika operesheni hiyo iliyoendelea hadi kesho yake nyumba 20 za raia wa Palestina ziliharibiwa na watu 60 waliokuwemo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo, wakauawa kwa umati.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 14 Februari mwaka 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia nchi mbili za Marekani na Uingereza zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya Ujerumani. Ndege 1773 za kijeshi zilitumiwa katika mashambulizi hayo ambayo ndiyo yaliyokuwa na hasara kubwa zaidi ya mali na nafsi duniani hadi hii leo. Mashambulizi hayo ya kinyama ya Marekani na Uingereza yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tatu yalisawazisha na ardhi miji kadhaa ya viwanda ya Ujerumani na kuifanya majivu matupu. Raia kati ya laki moja na nusu hadi laki mbili na nusu waliuawa kinyama katika mashambulizi hayo.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, Martin Scott tabibu mpasuaji wa Uingereza alifanikiwa kuunganisha figo ya mwanadamu. Siku hiyo Prf. Scott alichukua figo ya mtu aliyekuwa amefariki dunia na kuiunganisha kwa mafanikio na mgonjwa aliyekuwa amelazwa katika hospitali moja ya Leeds huko Uingereza.

Katika siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, aliuawa Rafiq Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon kwenye mlipuko wa bomu lililotegwa garini huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Alikuwa mmoja wa wafanyabiashara tajiri nchini Lebanon na wakati alipofariki dunia alikuwa na umri wa miaka 61. Hariri alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu wa Lebanon kutokea mwaka 1992, muda mfupi baada ya kumalizika vita vya ndani vya Lebanon hadi mwaka 1998, na kuchukua tena wadhifa huo mwaka 2000 hadi 2004.

Rafiq Hariri

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, ilianza harakati ya kupigania uhuru ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kiimla wa Aal-Khalifah. Tangu Bahrain ilipopata uhuru mnamo mwaka 1971, wananchi wa nchi nchi hiyo wamekuwa wakitaka uhuru na demokrasia ambavyo vimekuwa vikikandamizwa na utawala huo. Tangu wakati huo, Waislamu wa Kishia ambao ndio wanaounda asilimia kubwa ya raia wa nchi hiyo, wamekuwa wakibaguliwa, kukandamizwa na kunyimwa haki zao za kimsingi. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana kwa mara kadhaa harakati hizo za kupigania uhuru zikawa zinaibuka dhidi ya utawala huo wa Aal-Khalifah ambao una mafungamano na Saudi Arabia ya Kiwahabi huku ukiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata hivyo badala ya utawala huo kusikiliza matakwa ya wananchi umekuwa ukitumia mtutu wa bunduki na ukandamizaji wa kuchupa mipaka katika kuzima harakati hizo.

Harakati ya kupigania haki ya Bahrain