Jumatatu tarehe 15 Februari mwaka 2021
Leo ni Jumatatu tarehe tatu Rajab 1442 Hijria sawa na Februari 15 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 457 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba, sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba, ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na akahukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Miaka 239 iliyopita katika siku kama ya leo vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba, vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Bahman, idadi kadhaa ya viongozi wa utawala wa Kipahlavi walinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya usaliti na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Iran. Licha ya kuwa kwa mtazamo wa wananchi Waislamu wa Iran jinai za viongozi hao wa utawala dhalimu wa Shah zilikuwa wazi na bayana, lakini kwa amri ya Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu kuliundwa Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na kushughulikia kesi za viongozi hao waliokuwa wametiwa mbaroni na vikosi vya wananchi.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya Zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na muqawama wa mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.