Feb 15, 2021 23:10 UTC
  • Jumanne, tarehe 16 Februari, 2021

Leo ni Jumanne tarehe 4 Rajab mwaka 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Februari mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1992 Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi

Siku kama leo miaka 75 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya Zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili, alimu na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria katika eneo la Jabal Amili nchini Lebanon na kupata elimu ya msingi ya Kiislamu nchini humo. Ayatullah Sayyid Amin alielekea Najaf nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 24 kwa shabaha ya kukamilisha elimu ya juu na kupata elimu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Baadaye alielekea Syria na kutoa huduma kubwa za kufundisha Uislamu. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi muhimu zaidi kikiwa kile cha A'yanul Shia chenye juzuu kumi. Katika kitabu hicho Sayyid Muhsin al Amin amearifisha vinara wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia hususan maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na mchango wao katika kuimarisha ustaarabu wa Kiislamu. Kitabu kingine cha msomi huyo ni Kashful Irtiyab fii Atba'I Muhammad bin Abdul Wahhab kinachofichua na kukosoa itikadi za kundi potofu la Kiwahabi.

Ayatullah Sayyid Muhsin Amin al Amili

Na siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Bendera ya Lithuania